Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto kupitia vyama vya Ushirika AMCOS na Chama Kikuu ACU, Agosti 11,2024, imezindua mnada wa zao la mbaazi kupitia mfumo wa kidigitali wa TMX unaomuwezesha mkulima kuuza mazao yake kupitia mtandao ambapo ataweza kuuza kwa bei ya juu na kunufaika ili kuepuka walanguzi wa zao hilo.
Akizungumza na wakulima hao wa mbaazi Wilayani humo, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Remidius Mwema, amesema kuwa serikali imejipanga kumuinua mkulima wa mbaazi na kuhakikisha mkulima anauza mazao yake kwa faida. Aidha Mhe. Mwema amekemea vitendo vya baadhi ya walanguzi kupotosha juu ya mnada kupitia mfumo wa kidigitali.
"Ni muhimu kuwa wakweli kwa sababu lengo ni kumsaidia mkulima yeyote, kuna watu ni wakulima wakubwa wapo humu ndani wanaleta, lakini kwenda wewe kumlangua mtu ukaja wewe kunufaika hapa, inakuwa hutendi haki" DC Mwema.
Aidha, Meneja wa Chama Cha Msingi Matui AMCOS, Ndg. Emmanuel Keyaa, ameipongeza serikali kwa kuleta mfumo huu kwa wakulima wa mbaazi na kuomba ifanye hivyo kwa mazao mengine ili wakulima wafaidike.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi Biashara TMX, Shani Mringo, amesema lengo kubwa la mnada huo ni kuwakutanisha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa ndani na nje ya nchi ili kuweza kufanya biashara moja kwa moja kupitia mfumo wa kidigitali na muuzaji kulipwa kwa bei iliopo sokoni ndani ya masaa 48.
Wakizungumzia kufurahishwa na mfumo huo wa kidigitali wa kuuza zao hilo, baadhi ya wakulima na wauzaji hao wa mbaazi wameipongeza serikali kwa kuleta mfumo huo wenye tija kwa mazao yao.
Katika mnada huo wa kwanza katika msimu huu ambao umefanyika Agosti 11, 2024 katika kata ya Matui, jumla ya tani 116 za mbaazi zimeuzwa kwenye mnada huo kwa wanunuaji watatu tofauti kwa wastani wa bei ya TZS 2,127.78 kwa kila kilo.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa