Maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani yameanza rasmi leo Septemba 26, 2025 katika Wilaya ya Kiteto kwa kutoa elimu kwa wanafunzi kutoka shule 12, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa huo hatari.
Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo, Wizara ya Afya, halmashauri mbalimbali na kutoka sekta binafsi wametoa elimu kwa wanafunzi, ili kuwajengea uelewa juu ya namna ya kujikinga na madhara yatokanayo na ugonjwa wa kichaa cha mbwa.
Elimu iliyotolewa imejikita katika kueleza maana ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa, chanzo cha ugonjwa, jinsi unavyoambukizwa, dalili za mbwa mwenye maambukizi, dalili za mtu aliyepata kichaa cha mbwa pamoja na hatua za haraka za kuchukua endapo mtu atang’atwa na mbwa.
Aidha, wataalamu waliwahimiza wanafunzi hao kuwa mabalozi wa elimu hiyo katika jamii zao kwa kushirikisha wazazi, ndugu na marafiki ili kuongeza uelewa na kuchochea uwajibikaji wa pamoja katika kupambana na ugonjwa huo.
Wanafunzi pia walikumbushwa kujenga mazoea ya kuwapatia mbwa wao chanjo kwa kuzingatia utaratibu ulioweka na kwa sasa walihimizwa kutumia maadhimisho haya kuwapeleka mbwa na paka wao katika vituo vilivyoteuliwa ili kupata chanjo dhidi ya kichaa cha mbwa, hatua inayosaidia kulinda afya ya binadamu na wanyama.
Mbali na elimu, huduma mbalimbali za kiafya kwa wanyama zinatolewa katika kipindi hiki cha maadhimisho ikiwemo utoaji wa chanjo kwa mbwa na paka, kuhasi mbwa na paka dume, kutolewa kizazi mbwa na paka jike, utoaji wa dawa za minyoo, pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu afya za wanyama hao.
Kilele cha maadhimisho ya Kichaa cha Mbwa Duniani kitafanyika katika Uwanja wa Mpira Kibaya Septemba 29,2025.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa