Mtaalamu Toka OR-Tamisemi Bw. Chance Akifundisha Mfumo Huo Katika Mafunzo Hayo Kwa Vitendo Katika Ukumbi wa Maktaba ya Wilaya ya Kiteto Kama Anavyoonekana Kwenye Picha Hapo Juu.
Wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Wakiwa Katika Mafunzo Hayo Kwa Vitendo Katika Ukumbi wa Maktaba ya Wilaya ya Kiteto Kama Wanavyoonekana Kwenye Picha Hapo Juu.
------------------------------------ HABARI KAMILI ------------------------------------
Madeni Management Information System (Madeni MIS) ni mfumo wa kielektroniki wa kitanzania uliotengenezwa na OFISI YA RAIS - TAMISEMI ili kuweza kutumika katika upokeaji wa madeni ya watumishi wa serikali, uhakiki wa madeni hayo na ulipaji wa madeni hayo. Mfumo huu ni rafiki wenye tija kwa serikali na watumishi kwa ujumla.
Mfumo huu ili uweze kufanya kazi katika ngazi zote uwezeshwaji wa mafunzo ni muhimu sana ambapo ngazi ya kitaifa tayari walishafanya na sasa ni ngazi ya Wilaya ambapo wataalamu toka OR-TAMISEMI Bw. Chance na Bw. Faustine wamewawezesha wataalamu wa Halmashauri ya wilaya ya kiteto kwa muda wa siku 2 kuanzia tarehe 31.08.2020 hadi 01.09.2020 kwa Mkurugenzi mtendaji wa Wilaya, Maafisa Elimu Msingi na Sekondari, Maafisa Utumishi, Wakaguzi wa ndani, Wahasibu na Maafisa Tehama. Kwa sasa mfumo huu utaanza kwa kada ya elimu msingi na sekondari kwani watumishi wa sekta hii ni sawa na 52% ya watumishi wote wa Tanzania kisha baadaye utatumika kwa watumishi wote wa serikali.
Malengo ya mfumo huu wa kielektroniki ni kutatua changamoto za usimamizi wa uhakika na ufuatiliaji wa malipo ya madai ya watumishi yasiyohusu mishahara ambapo hapo awali rasilimali nyingi sana zilikuwa zinatumika katika kuhakiki kwa usahihi madeni husika, ukosefu wa uwazi na uwajibikaji ambapo matokeo chanya yanayotegemewa ni kupunguza malalamiko ya watumishi, kuongeza moyo wa kufanya kazi na hatimaye kuongeza ufanisi wa shuguli za sekta husika.
Kimsingi mfumo huu utahitaji mtumishi husika kuanzisha madai yake mwenyewe katika kituo chake cha kutolea huduma bila usumbufu wa kusafiri kwenda Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri husika kuwasilisha madai yake kwa kuwa kila atakachokifanya mwalimu mkuu wa shule aliyepo mwalimu atapokea na kuchambua kisha madai haya atayawalisha katika ngazi ya wilaya kwa uchambuzi zaidi na malipo. Katika hatua zote hizi mtumishi mwenye madai husika atakuwa anaona hatua kwa hatua kila kitakachokuwa kinafanyika kwenye mfumo na kwa uwazi zaidi ukiacha madai ya nyuma.
Kwa mfumo huu kila mtumiaji atakuwa na uwezo wa kuona ripoti mbalimbali kulingana na cheo chake, ikiwemo jumla ya waalimu wanaodai, madai na madeni yaliyopo, jumla ya madai na madeni yaliyolipwa na mengineyo.
Mfumo huu tayari umeshaanza kutumika kuanzia tarehe 01.09.2020 katika ngazi ya Halmashauri kwa kuingiza madeni ya nyuma yaliyohakikiwa ambayo yapo kwenye faili la mtumishi husika kisha kuanzia mwezi Oktoba 2020, baada ya mafunzo kwa waalimu kukamilika ndipo kila mwalimu ataweza kuingiza madai yake mwenyewe kwa utaratibu maalumu atakaopewa akiwa nyumbani kwake au katika kituo cha kazi au popote pale kwa kutumia simu, kompyuta mpakato, kompyuta na vifaa vingine vya kielektroniki vyenye uwezo wa kufanya kazi kama hizi cha msingi kifaa husika kiwe kimeunganishwa na wavuti "internet" na pia muhusika awe ameshasajiriwa kwenye mfumo huu.
Tunaishukuru sana, serikali ya awamu ya 5 inayoongozwa na Mh. Rais Dkt J.P.Magufuli kwa kuwa sikivu katika kutatua kero za watumishi kwa kutumia teknolojia hii ya mifumo ya kielektroniki ya kompyuta ili kuepusha usumbufu kwa watumishi katika uwazi wa ufuatiliaji wa madai husika, kutembea kwa kutumia fedha nyingi na muda wa kuhudumia wananchi katika maeneo yao utaongezeka.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa