Katika mwili wa binadamu, ini ni kiungo muhimu kinachohusika na kuchuja na kuondoa sumu zinazotengenezwa mwilini, kumeng’enya virutubisho, kutengeneza nyongo na protini na pia ini linahusika kwenye kinga ya mwili. Miaka ya hivi karibuni, kiungo hiki kimekua hatarini kutokana na kuenea kwa maambukizi yanaojulikana kama Homa ya Ini (Hepatitis).
Homa ya ini (Hepatitis) ni ugonjwa wa maambukizi unaosababisha uvimbe kwenye ini kutokana na maambukizi ya virusi. Ugonjwa huu umegawanyika katika makundi A mpaka E ambapo kundi A na E husababisha madhara ya muda mfupi kwenye ini wakati kundi B,C na D inasababisha madhara ya muda mfupi na muda mrefu.
Katika makundi yote hayo kundi B (Hepatitis B) imetajwa na wataalamu wa afya kuwa ni hatari zaidi na na hivyo makala hii inajikita zaidi kutoa elimu kuhusu kundi hilo kwani huathiri watu wengi zaidi.
Kwa mujibu wa daktari kutoka katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto Dkt. Honest Michael, kutokana na takwimu za watu wanaojitolea damu wilayani hapa, katika kila watu 100 wanaopimwa Hepatitis B, watu wanne hupatikana na maambukizi ya Hepatitis B. Takwimu hizi zinaashiria kwamba ugonjwa huu upo karibu nasi.
NJIA YA MAAMBUKIZI.
Virusi vya Hepatiis B huenezwa kupitia damu au aina zote za maji maji yanatengenezwa mwilini ikiwemo mate, maji maji yanatoka ukeni pamoja na mbegu za kiume. Kutokana na hayo njia kuu za mambukizi ya virusi vya Hepatitis B ni pamoja na kufanya ngono bila kinga, kuchangia sindano au vitu venye ncha kali, kuchangia miswaki, kuongezewa damu isiyo salama pamoja na kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua au wakati wa kunyonyesha.
DALILI ZA MAAMBUKIZI YA HOMA YA INI
Dalili za maambukizi ya Homa ya Ini kwa kiasi kikubwa hufanana na dalili za homa za kawaida hivyo mtu apatapo dalili hizo anaweza kudhani amepata homa za kawaida. Dalili hizo ni pamoja na uchovu wa mwili, kutapika, kuharisha, maumivu ya tumbo, pamoja na mabadiliko ya ngozi au macho kuwa ya njano.
MATIBABU YA HEPATITIS B
Mwili wa binadamu una uwezo wa kutengeneza kinga na kupambana na maambukizi ya homa ya ini endapo ugonjwa huo upo kwenye hatua za awali. Hivyo watu wanaopatikana na maambukizi hayo wataalamu wa afya hushauri kuzingatia kanuni bora za maisha ikiwa ni pamoja na kula vyakula bora, kufanya mazoezi, kuepuka matumizi ya pombe pamoja na kujilinda kupata maambukizi mapya. Takwimu zinaonesha kwamba katika watu 100 wenye Hepatitis B, asilimia 95 hupona kwa kutengeneza kinga mwilini huku asilimia 5 miili yao hushindwa kutengeneza kinga na kuwafanya wabaki na maambukizi ya muda mrefu yanayohitaji tiba ili kuzuia madhara
Kwa wagonjwa wanaoshindwa kupambana na maambukizi hayo ya Hepatitis B matibabu yao hutegemea hatua mgonjwa aliyofikia, na wakati mwingine hulazimika kutumia dawa maalumu zinazozuia uzalishaji wa virusi hivi ili kuipa kinga ya mwili nafasi ya kuviondoa.
MADHARA YA HEPATITIS B
Endapo mgonjwa atachelewa kuanza matibabu mapema ugonjwa huu huweza kuleta madhara mbalimbali ikiwa ni pamoja na ini kusinyaa (cirrhosis) na kupelekea kushindwa kufanya kazi, kusababisha kansa ya ini na pia huweza kupelekea kifo.
NJIA ZA KUJIKINGA.
Mtu anaweza kujilinda dhidi ya Hepatitis B kwa kuepuka kufanya ngono isiyo salama, kuepuka kuwa na wenza wengi, kujenga tabia ya kupima afya haswa kuangalia kama ana maambukizi ya Hepatitis B pamoja na kupata chanjo ya Hepatitis B.
UTOAJI WA CHANJO YA HEPATITIS B
Serikali imewezesha upatikanaji wa chanjo ya Hepatitis B katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa gharama nafuu. Wilayani Kiteto chanjo hii hutolewa katika Hospitali ya wilaya. Chanjo hiyo hutolewa katika dozi tatu ambapo dozi ya kwanza hutolewa wakati wowote, dozi ya pili baada ya mwezi mmoja na dozi ya tatu baada ya miezi sita.
Kabla ya chanjo, ni lazma kupima ili kubaini kama mtu ana maambukizi ya Hepatitis B na endapo atakutwa hana maambukizi ndipo huanzishiwa chanjo.
MUITIKIO WA WANANCHI KITETO DHIDI CHANJO YA HEPATITIS B NA WITO WA MTAALAMU WA AFYA
Kwa mujibu wa Dkt. Honest, muitikio wa wananchi wa Kiteto juu ya kupata chanjo ya Hepatitis B bado hauridhishi, hivyo ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwenda kupima ugonjwa huo na kupata chanjo.
“Ninatoa wito kwa wananchi kuja kupima ili wajue kama wana maambukizi ya Hepatitis B ama hawana. Gharama za kupima shilingi 10,000 na kila dozi inagharimu shilingi 10,000 hivyo jumla hapo ni 40,000. Gharama hii ni ndogo ukilinganisha na matibabu ya Hepatitis B”, amesema Dkt. Honest.
Wataalamu wa afya wanasema kila mtu yupo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya Hepatitis B. Hivyo wananchi wanashauriwa na kuhimizwa kuchukua hatua mapema kupima afya zao na kupata chanjo ili kujilinda maana KINGA NI BORA KULIKO TIBA.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa