Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhe. Remidius Mwema, ametoa rai kwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto kukemea kwa nguvu zote dhana ya ukabila na kuwasisitiza viongozi hao kulinda umoja na mshikamano wa wananchi bila kuwagawa kwa misingi ya asili zao.
Akizungumza Desemba 2, 2025 katika Mkutano wa Kwanza wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Mhe. Mwema ameeleza kuwa ukabila unaweza kuwa chanzo cha mafarakano wikayani haoa hivyo ni wajibu wa viongozi viongozi hao kuhakikisha dhana hiyo inakomeshwa.
“Waheshimiwa madiwani, nendeni mkakemee dhana ya ukabila, mtu akikosea ajulikane kwa jina lake si kwa kabila lake”, alisema Mhe. Mwema
“Muasisi wa taifa alikemea ukabila, nasi kama viongozi hatuna budi kuukemea kwa vitendo,” aliongeza Mhe. Mwema.
Katika Mkutano huo , waheshimiwa madiwani walikula Kiapo cha Udiwani mbele ya Mheshimiwa Hakimu Boniface Lihamwike, Hakimu Mkazi Mkuu. Aidha, madiwani hao pia walitoa Ahadi ya Uadilifu wa Viongozi mbele ya Ndg. Josephat Mkumbwa kwa niaba ya Kamishna wa Maadili.

Mhe. Mwema amewataka madiwani kuwa mstari wa mbele katika utatuzi wa changamoto za wananchi, badala ya kuwa sehemu ya migogoro. Amewasisitiza kusimamia na kuwaelimisha wananchi juu ya mpango wa matumizi bora ya ardhi, akibainisha kuwa migogoro mingi ya ardhi imekuwa ikichochewa na mgawanyiko unaoweza kuzuilika.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kushughulikia migogoro yote ya wilayani Kiteto, na hivyo kabla ya kuanza kutatua changamoto zozote, madiwani wahakikishe wanafahamu hatua za sasa za mchakato wa utatuzi wa migogoro hiyo.
Awali, Mhe. Mwema aliwapongeza madiwani wote kwa kuaminiwa na wananchi. Kipekee alimpongeza Mhe. Athumani Hamisi Kilimo kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto na Mhe. Abdala Bundala, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza lililopita, kwa kuliongoza baraza hilo kwa hekima na busara kwa kipindi cha miaka mitano.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa