Wahe. madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto wakimsikiliza Mkuu wa wilaya wakati akitoa maelezo ya serikali kwenye kikao cha baraza lilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akizungumza wakati wa kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Mhe. Lairumbe Mollel akifungua kikao cha baraza la madiwani,kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri.
...........HABARI KAMILI................
Mkuu wa wilaya ya Kiteto mheshimiwa Tumaini Magessa amewataka waheshimiwa madiwani kuhimiza elimu kwenye kata zao.Mhe Magessa ameyasema hayo katika siku ya pili ya kikao cha baraza la madiwani lililofanyika tarehe 30 -31 Januari 2019 katika ukumbi wa Halmashauri.
Akizungumza wakati akitoa maelekezo ya serikali ,Mhe. Magessa amesema “Ninyi ndio madiwani, kila mmoja anasimamia maendeleo ya kata yake, zile WDC mnazokaa mhimize elimu. ili maendeleo yaweze kutokea, ni lazima Kiteto ipige hatua za kwenda mbele katika suala la elimu”.
Kadhalika Mhe. Magessa amezungumzia kuhusu suala la kilimo ambapo amesisitiza juu ya azma yake ya kuhakikisha kwamba kilimo kinachofanyika wilayani hapa kinakuwa ni kilimo cha kisasa. Katika kuhakikisha kwamba utekelezaji wa agizo hilo unafuatiliwa, Mhe. Magessa amemuagiza afisa kilimo wilaya kwa kushirikiana na maafisa wa idara yake kufanya ufuatiliaji kwa kuanzia kwa wakuu wa idara za Halmashauri na taasisi nyingine za serikali zilizopo wilayani hapa na kutoa taarifa kwake ,ili yeye pamoja na kamati yake ya ulinzi na usalama wapate pa kuanzia.Amesisitiza kwamba utekelezaji usipofanyika kwa vitendo itaonekana kwamba hakuna kitu kinachofanyika.
Mhe. Magessa pia mewataka wakuu wa idara kuungana katika utendaji wa kazi ili kupunguza gharama za uendeshaji.Akitoa ufafanuzi kuhusu maelekezo hayo Mhe Magessa amesema kwamba kama wakuu wa idara watatu au wanne wana ratiba ya kwenda kufanya kazi katika kata au kijiji fulani kwa siku moja, badala ya kila mkuu wa idara kuondoka na gari yake ,wote wanaweza kutumia gari moja ,wakaenda kufanya kazi huko, wakimaliza wanarudi pamoja.
Amesisitiza kwamba ushirikiano wa wakuu wa idara ni muhimu katika kufanya kazi kwa ufanisi na kwa ghrama ndogo,kuliko kila mtu akifanya kivyake.Hivyo ni vema utaratibu ukawekwa,na mawasiliano yakawekwa vizuri ili jambo hilo liwezekane.
Katika hatua nyingine mwenyekiti wa Halmashauri Mhe Lairumbe Mollel amewataka Waheshimiwa madiwani kuhakikisha kwamba fedha za mfuko wa jimbo zilizokwenda katika kata zao kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa miundo mbinu mashuleni ,zinatekeleza miradi hiyo kwa wakati. Ili watoto waweze kusoma katika mazingira yanayofaa.Amesisitiza kwamba isifike mwezi wa nne fedha hizo zikiwa bado hazijatumika.
Suala la elimu limekuwa ni moja wapo ya vipaumbele kwa uongozi wa wilaya ya Kiteto.Kutokana na hali ya matoke ya kidato cha nne mwaka 2018, mkuu wa wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri wameazimia kukaa pamoja na walimu wakuu,walimu wa taaluma,waratibu elimu kata na watumishi wa idara ya elimu ngazi ya wilaya ili kujadili kwa pamoja changamoto na namna watakavyoweza kuinua kiwango cha ufaulu wilayani hapa,husuani kwa upande wa sekondari.
..............MWISHO......................
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa