Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Kiteto, CPA. Hawa Abdul Hassan, amewaasa Waandishi Wasaidizi na Waendesha Vifaa vya Bayometriki kufanya kazi kwa kufuata sheria ,taratibu na miongozo.
Rai hiyo imetolewa Mei 14, 2025 wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa Maafisa hao yenye lengo la kuwajengea uwezo maafisa hao kwenye ujazaji wa fomu mbalimbali pamoja na kuwajengea uwezo wa utumiaji wa mifumo na vifaa vya uandikishaji kwenye zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili wilayani hapa zoezi ambalo linatarajiwa kufanyika Mei 16-22, 2025.
Aidha CPA. Hawa amesema kwamba ana imani maafisa hao watafanya kazi kwa ueledi na moyo wa kujituma ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu ili kuweza kufikia malengo.
Mbali kufanya kazi kwa bidii na kujituma, aliwaasa pia juu ya utunzaji mzuri wa vifaa watakavyoenda kuvitumia.
Kabla ya kuanza mafunzo hayo, maafisa hao walikula kiapo cha kujivua uanachama wa siasa na kiapo cha kutunza, viapo ambavyo waliapa mbele ya Afisa Mwandikishaji huyo.
Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili, litaenda sambamba pamoja na uwekaji wazi wa daftari la awali la wapiga kura hivyo wananchi wanahimizwa kwenda kuhakiki taarifa zao kwenye vituo walivyojiandikisha na endapo watazikuta zinadosari wanapaswa kuboresha taarifa zao.
Wananchi ambao hawakujiandikisha au hawakuboresha taarifa zao katika zoezi la awali wanahimizwa pia kushiriki zoezi hili ili waweze kupata sifa ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
"Kujiandikisha kua Mpiga Kura, ni Msingi wa Uchaguzi Bora".
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa