Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya Kiteto, CPA. Hawa Abdul Hassan kwa niaba ya marafiki zake, amekabidhi madawati 70 yenye thamani ya shilingi 5,600,000 kwa Mkuu wa Wilaya Kiteto, Mh. Remidius Mwema Emmanuel, kwaajili ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati wilayani hapo.
Akiongea katika hafla ya makabidhiano ya madawati hayo iliyofanyika katika Shule ya Msingi Kaloleni Januari 31, 2024, Mkurugenzi huyo alisema kwamba baada ya kuteuliwa na kufika Wilayani Kiteto alikuta kuna mpango mkakati wa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati; mpango ambao ulizinduliwa 2.11.2022 na aliyekua Mkuu wa Wilaya Kiteto SSI Mbaraka Alhaji Batenga.
“Huu mkakati niliupenda na nikaona ni vyema niunge mkono juhudi za Rais Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na juhudi za Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kuwashirikisha marafiki zangu na kuwaomba wanichangie chochote walichojaliwa ili tuweze kupata madawati kwaajili ya wanafunzi wetu wa Kiteto na hatimaye leo kwa niaba ya marafiki zangu ninakabidhi madawati haya”.
Aidha Mkurugenzi huyo amewashukuru marafiki zake kwa kumuunga mkono na kuwezesha kupatikana kwa madawati hayo 70 ambayo yatakaliwa na wanafunzi 210 ambao walikua wanakaa chini wawapo darasani.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mh. Mwema, ambaye ndiye aliyekua Mgeni Rasmi katika hafla ya makabidhiano, aliwashukuru Marafiki wa CPA. Hawa Abdul Hassan kwa mchango wao na alisema kwamba Ofisi ya Mkuu wa Wilaya inathamini mchango wao huo.
Aidha Mh. Mwema alisema kwamba maana ya kiongozi ni kuongoza njia hivyo alimpongeza Mkurugenzi huyo kwa kuunga mkono mkakati huo na alitoa wito wa viongozi wengine kuiga mfano huo.
Kabla ya kuanza kwa mpango mkakati huo wa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati, Wilaya ya Kiteto ilikua na upungufu wa madawati 9,023 kwa shule za msingi ila kwa sasa wilaya ina upungufu wa madawati 7,702. Hivyo Mh Mwema alitoa wito wa viongozi wengine na wadau mbalimbali kuiga mfano wa Mkurugenzi CPA. Hawa.
“Viongozi wengine wote tuige mfano wa Mkurugenzi . Kila mmoja akitafuta rafiki zake wa kutosha tunaweza kumaliza au kupunguza tatizo hili kwa asilimia kubwa”, alisema Mh. Mwema.
Madawati 70 yaliyotolewa na Marafiki wa CPA. Hawa Abdul Hassan, 50 ni kwaajili ya shule ya Msingi Enguserosidan iliyopo kata ya Laiseri na madawati 20 ni kwa ajili ya Shule ya Msingi Olchaniodo iliyopo kata ya Partimbo.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa