Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya ya wanyama imeandaa Mpango Rasmi wa kutokomeza Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa ikiwa ni moja ya mkakati wa kufikia azma ya Dunia ya kuondokana kabisa na ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi Agnes Meena katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Kitaifa yaliyofanyika leo Septemba 29, 2025 Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara.
Bi. Meena amesema kwamba mpango huo ambao umeshapitiwa na kuridhiwa na Shirika la Afya ya Wanyama duniani (WOAH) unalenga utaratibu wa uchanji wa mbwa na paka wote nchini kwa muda wa miaka mitano.
“Kupitia mpango huo, ni imani yetu kwamba hadi kufikia mwaka 2030 Tanzania itakua ni miongoni mwa nchi zitakazokuwa zimeutokomeza ugonjwa huu wa Kichaa cha Mbwa”,amesema Bi Meena.
Vilevile amesema kuwa mbwa, paka na wanyama wengine wakitunzwa vizuri wana umuhimu katika maisha ya kila siku ya binadamu huku akiongeza wasipopewa chanjo ya magonjwa hususani kichaa cha mbwa wanyama hao wanageuka kuwa hatari kwa binadamu.
“Kwa hiyo lengo la maadhimisho haya ambayo yamesababisha tukusanyike hapa leo ni kukumbushana na kuelimishana zaidi jinsi ya kukabiliana na janga hili la ugonjwa wa kichaa cha mbwa”, amesema Bi Meena.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Wanyama wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Benezeth Lutege amebainisha kuwa takwimu zinaonesha katika maadhimisho wilayani hapa mpaka kufikia Septemba 29, 2025 wametoa chanjo kwa Mbwa 3653, Paka 212, Kuhasi Mbwa 96, Paka 5 na Kufunga Vizazi Mbwa 52, Paka 26.
Akisoma taarifa ya Wilaya, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto Bi. Mufandii Msaghaa amesema kwamba wilaya ya Kiteto imejitahidi kuzitekelza sera za serikali kuhusu mifugo hususani kuthibiti magonjwa ya wanyama.
“Serikali imejitahidi kuthibiti magonjwa kwa kutoa kinga ya magonjwa ya wanyama. Kila mwaka wataalam wetu wamekua wakitoa huduma ya chanjo kama sera zinavyotutaka”, amesema Bi. Msaghaa.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa