Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, amewahimiza wazee kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza leo Oktoba 7, 2025, katika Maadhimisho ya Siku ya Wazee yaliyofanyika katika Kata ya Kibaya kwa ngazi ya Wilaya,Mhe. Mwema amesema wazee wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko chanya kupitia sanduku la kura, hivyo wasikose kushiriki kwa mujibu wa kauli mbiu ya mwaka huu isemayo: “Wazee Tushiriki Uchaguzi Mkuu kwa Ustawi wa Jamii Yetu.”
Aidha, aliwasihi wazee kutumia nafasi yao ya heshima na uzoefu kuwashauri vijana kushiriki kikamilifu katika uchaguzi na shughuli za kijamii, alieleza kuwa ni njia bora ya kuwajenga kimaadili na kuwaepusha na makundi hatarishi.
“Ofisi yangu iko wazi, msisite kufika kunishauri au kunieleza changamoto mnazokutana nazo. Niko tayari kushirikiana nanyi kwa maendeleo ya Kiteto na Taifa kwa ujumla,” aliongeza Mhe. Mwema.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, CPA. Hawa Abdul Hassan, alitumia maadhimisho hayo kupongeza mchango wa wazee katika ustawi wa jamii, akibainisha kuwa Serikali inaendelea kuwajali na kutekeleza sera rafiki kwao.
“Tunamshukuru Mungu kwa kutupa wazee hawa, kwani wazee ni dawa na faraja kwa vijana,tumehuisha baraza la wazee na tayari tumeanza na vikao. Mapendekezo yote yaliyowasilishwa leo, yale yasiyo hitaji fedha tutayafanyia kazi mara moja, na yanayohitaji fedha tutaanza kuyashughulikia kuanzia sasa,” alisema CPA. Hawa.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Bi. Jackline Barongo, aliisihi jamii kuendeleza utamaduni wa kuenzi wazee kama nguzo muhimu ya jamii, akisisitiza umuhimu wa kutambua mchango wao katika kujenga taifa lenye maadili.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa