Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ndg. Ismal Ali Ussi, ameipongeza Kiteto kwa kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Pongezi hizo zimetolewa Julai 13, 2025 mara baada ya kukabidhi mitungi 50 ya gesi ya kupikia kwa makundi matatu ambayo ni wajasiriamali (10), zahanati (1), Shule za Msingi (29) na Shule za Sekondari (10). Mitungi hiyo yenye thamani ya TZS 3,800,000, imekabidhiwa katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ndedo mara baada ya Mwenge wa Uhuru kupokelewa wilayani hapa katika viwanja hivyo.
Kiteto inafanya uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia kwa jamii wilayani hapa ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali na wadau wa maendeleo katika kulinda mazingira na kuboresha afya. Katika kutekeleza adhma hii, Halmashauri kupitia Kitengo cha Mazingira, imeweza kutoa elimu shuleni, vikundi vya jinsia na rika tofauti kwenye jamii, kushirikiana na wadau wa maendeleo na kufadhili na kusambaza majiko banifu pamoja na kutoa mafunzo kwa jamii kuhusu namna ya kuyatumia, kuwajengea uwezo wajasiriamali wa nishati safi kupitia mafunzo yaliyotolewa kwa wajasiriamali wanaohusika na utengenezaji na matengenezo ya majiko banifu na vifaa vya LPG(Liquefied Petroleum Gas) ili kuongeza ufanisi na usalama vinapotumiwa na wananchi.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Ndg. Ussi ameipongeza Wilaya ya Kiteto kwa juhudi za kuiunga serikali mkono kwenye mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Napenda kutumia nafasi hii kuwapongezeni kwa jitihada mnazozionesha katika kuunga mkono juhudi za Rais Samia juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia. Matumizi ya kuni yalikua yanamnyima usingizi Rais Samia”, alisema Ndg. Ussi.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa