Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Lerug wilayani Kiteto ,ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo ya jimbo lake.
Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian ,uongozi wa CCM wilaya ya Kiteto, viongozi wa kata na kijiji pamoja na wazee wa mila wakikagua vyumba vya madarasa vilivyojengwa kwa ajili ya shule ya msingi ya kijiji cha Lerug.
Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian ,uongozi wa CCM wilaya ya Kiteto, viongozi wa kata, viongozi wa kijiji na wazee wa mila wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Wanakijiji wa Lerug wakiwa wamekusanyika kumsikiliza mbunge wao katika mkutano wa hadhara.
Wanakijiji wa Lerug wakiwasilisha kero kwa mbunge wao katika mkutano wa hadhara.
....... HABARI KAMILI.......
Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian ameahidi kuchangia ujenzi wa madarasa kwa ajili ya shule ya msingi katika kijiji cha Lerug.Mhe. Papian ametoa ahadi hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Lerug wakati wa ziara yake kijijini hapo .
Akizungumza katika mkutano huo Mhe. Papian amesema kwamba aliahidi shilingi millioni moja kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, lakini anaongeza shilingi 500,000, iwe 1,500,000, na kwamba atanunua saruji ya kiasi hicho cha fedha,na kuiwasilisha kijijini hapo ili kuendeleza kazi ya ujenzi. Aidha Mhe. Papian amewahimiza wanakijiji wa Lerug kuendelea kuchangia ujenzi ,Mhe. Papian amesema “ Kwenye ile harambee sikuweza kuja, lakini nilituma mwakilishi. Ninyi mmefanya kazi kubwa sana mpaka hapa madarasa yalipofika,tunawapongeza sana, lakini msiishie hapo. Endeleeni kushikamana kuchangia mpaka idadi ya majengo yanayotakiwa itakapokamilika”.
Kadhalika Mhe. Papian ameahidi kushughulikia tatizo la maji, tatizo ambalo ndio kero kubwa kwa wanakijiji,ili kuhakikisha kwamba maji yanapatikana katika kijiji hicho sambamba na kushughulikia ubovu wa barabara, ambapo amesema kwamba atazungumza na watu wa TARURA,ili barabara kubwa inayoingia kijijini hapo iweze kutengenezwa.
Vilevile Mhe. Mbunge amemuagiza Mtendaji wa kijiji hicho kuhakikisha kwamba wanakijiji wote wanapimiwa maeneo ili waweze kujenga nyumba bora za kuishi pamoja na vyoo, na katika upimaji huo kusiwe na ubaguzi wa aina yoyote.Pia ametoa rai kwa wafugaji wa kuacha tabia ya kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima,badala yake wao pamoja na wakulima waishi kwa upendo na maelewano, wawe na utaratibu wa kusubiri mazao yatolewe shambani, baada ya mazao kutolewa wafanye makubaliano ya kupeana mabua ili kudumisha amani kati yao na kutowasababishia wakulima hasara.
Mpaka sasa, wanakijiji wa Lerug wameweza kujenga madarasa manne na ofisi moja ,madarasa mawili na ofisi yakiwa yameshapauliwa na mawili yakiwa katika hatua ya lenta. Majengo hayo yote yamejengwa kwa nguvu za wananchi.
...........MWISHO............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa