Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian akizungumza na wanakijiji wa Ngapapa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake kukagua shughuli za maendeleo na kusikiliza kero za wapiga kura wake.
Diwani wa kata ya Kijungu Mhe. Mandaro Mussa akizungumza katika mkutano huo.
Mtendaji wa kijiji cha Ngapapa Ndg. Gerald M. Dani akitambulisha uongozi wa serikali ya Kijiji chake katika mkutano huo .
Wakazi wa kijiji cha Ngapapa wakiwa wamekusanyika katika mkutano huo kumsikiliza Mhe. Mbunge .
Wakazi wa kijiji cha Ngapapa wakiwasilisha kero zao kwa Mhe. Mbunge.
............... HABARI KAMILI................
Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe .Emmanuel Papian amewataka wakazi wa kijiji cha Ngapapa ,kata ya Kijungu wilaya ya Kiteto kuishi kwa amani na ushirikiano.Badala ya kuendeleza chuki na ubaguzi miongoni mwao.Mhe . Papian ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho.
Akizungumza katika mkutano huo Mhe. Papian amesema “ hatutaki kusikia mtu amelisha mifugo kwenye shamba la mwenzake. “kuchungia mifugo kwenye mashamba , wakati mazao bado yako shambani kunasababisha hasara kwa wakulima,na kujenga chuki kati ya wakulima na wafugaji.Tunataka amani na maendeleo, hatutaki chuki, hatutaki ubaguzi,msiendekeze suala la kubaguana, ni baya sana kwa sababu ,mnapanda mbegu ambayo mavuno yake ni uharibifu na laana.Kila binadamu anastahili kuheshimiwa na kutokubaguliwa”.
Kadhalika Mhe Papian amewaasa wakazi wa kijiji hicho ambao wanaendekeza tabia ya ulevi ,kuacha tabia hiyo, badala yake, wajikite zaidi katika shughuli za kuzalisha kipato ili waweze kujenga nyumba bora,wajiendeleze kimaisha na kuchangie miradi ya maendeleo katika kijiji chao, ili kijiji hicho kiwe na maendeleo.
Katika mkutano huo pia wanakijiji wa Ngapapa wamewasilisha kero zao kwa Mhe. Papian, kero namba moja ikiwa ni ukosefu wa chanzo cha maji,ambapo wamesema kwamba tatizo la maji ni kero kubwa sana kwao.Kero nyingine ni baadhi ya wakazi wa kijiji hicho ni kutokuwa na makazi baada ya makazi yao kuvunjwa,kwa madai ya makazi hayo kujengwa eneo lisiloruhusiwa.
Akijibu kuhusu kero ya maji Mhe. Papian amesema kuwa amesikia tatizo hilo , katika bajeti ijayo watafanya utaratibu ili kijiji hicho kiweze kupata walau kisima kimoja wakati mipango mingine ya kutafuta vyanzo vingine vya maji katika eneo hilo ikiwa inaendelea.Vilevile Mhe. Papian ameahidi kuzungumza na shirika lisilo la Kiserikali la KINAPA ili katika miradi yao ya kuchimba visima vya maji kwa ajili ya kusaidia vijiji waangalie uwezekano wa kuchimba kisima katika kijiji cha Lerug au Ngapapa, eneo hilo liwe na chanzo cha maji, na serikali itakapochimba kisima kingine ,viwepo visima viwili, maji yapatikane kwa watu wote.
Kuhusu kero ya baadhi ya wakazi wa kijiji hicho kutokuwa na makazi baada ya makazi yao kuvunjwa Mhe Papian ametoa maelekezo kwa afisa Mtendaji wa kijiji hicho ndugu Gerald M. Dani ,Mhe. Papian amesema “Moja wapo ya mambo ambayo lazima yafanyike , ni kufanya takwimu, kujua idadi ya watu ambao hawana viwanja, ambao ni wakazi wa kijiji hiki.Mtendaji fanya takwimu ya hawa waliokuwepo,na mpango wa matumizi bora ya ardhi wa hapa uujue, serikali ya kijiji mkae, mpange, watu wote wapate viwanja, mahali pamoja na bila ubaguzi kwamba huyu ni nani na yule ni nani, wajenge, ili iwe rahisi kuleta huduma.Eneo la makazi liwe ni hapa, waende mashambani wakalime ,warudi hapa.Waende machungani wakachunge mifugo yao, warudi hapa, ili huduma zote tulete hapa,kijiji hiki kiweze kuendelea”.
Mhe Papian amezuru katika kijiji cha Ngapapa ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo ya jimbo lake, sambamba na kusikiliza kero za wananchi wa jimbo lake kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi.
..............MWISHO..............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa