Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Ndedo.wakati alipotembelea shuleni hapo,ikiwa ni sehemu ya ziara yake kukagua shughuli za maendeleo jimboni mwake.
Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian akisaini katika kitabu cha wageni cha shule ya sekondari Ndedo.
Majengo kwa ajili ya Kituo cha afya Ndedo.
Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian akikagua ujenzi wa choo katika Kituo cha afya Ndedo.
Mabweni mawili yanayojengwa katika shule ya msingi Ndedo,yakiwa katika hatua ya upauzi.
Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian akikagua ujenzi wa mabweni katika shule ya msingi Ndedo.Waliosimama pembeni yake ni katibu wake,diwani wa kata ya Ndedo,kaimu mwenyekiti wa kijiji na Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Ndedo.
Wakazi wa kijji cha Ndedo wakiwa wamekusanyika kumsikiliza Mbunge wao Mhe Emmanuel Papian, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Ndedo
Wakazi wa kijji cha Ndedo wakiwasilisha kero kwa Mbunge wao Mhe Emmanuel Papian, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Ndedo
...........HABARI KAMILI............
Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papiani amemtaka mkuu wa shule kwa kushirikiana na uongozi wa kata ya ndedo na tarafa kuhamasisha wakazi wa kata ya Ndedo kuchangia ujenzi wa majengo kwa ajili ya kuanzisha kidato cha tano na cha sita katika shule ya Sekondari Ndedo.Mhe. Papian ameyasema hayo wakati akizungumza na mkuu wa shule ya sekondari ndedo,alipotembelea shuleni hapo katika zira yake aliyoifanya katika kata ya Ndedo mwanzoni mwa mwezi huu .
Akizungumza na mkuu wa shule hiyo mwalimu Nicomed Kwahison Mhe. Papian ameshauri kuandaliwa kwa harambee kubwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na mabweni, na kwamba harambee hiyo isimamiwe na katibu tarafa, watendaji wa kata na watendaji wa vijiji. Akisisitiza kuhusu hilo Mhe Papian amesema “Andaeni harambee, shirikianeni na katibu tawala na watendaji wote. Kila mtu achangie,wakwenda mnadani kuuza ng’ombe aende, wa kuuza mazao aueze, watu wachangie, na watendaji wote washiriki kukusanya hiyo michango,majengo kwa ajili ya kidato cha tano na sita yajengwe hapa.”
Naye Mwl. Kwahison amemueleza Mhe. Mbunge kuhusu tatizo la nyumba za walimu katika shule hiyo,ambapo amesema kwamba shule hiyo ina uhaba wa nyumba za walimu , na kwamba walimu wawili wamelazimika kuishi katika ofisi za kata.
Aidha Mhe. Papian amekagua ujenzi wa mabweni mawili katika shule ya msingi Ndedo, ambapo amepongeza kazi iliyofanyika, amesema kwamba wameitendea haki fedha iliyotolewa kwa ajili ya ujenzi wa mabweni hayo, sambamba na kumtaka mwalimu mkuu wa shule hiyo pamoja na kamati ya shule kuhakikisha kwamba mabweni hayo yanakamilika kwa wakati ili kupungumza msongamano wa wanafunzi kwenye mabweni sambamba na kuwawezesha wanafunzi wengine ambao wamekosa nafasi ya bweni na wanaishi mbali na shule kupata nafasi ya kulala katika mabweni hayo.
Katika hatua nyingine Mhe. Papian amezungumza na wakazi wa Ndedo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Ndedo,ambapo ameahidi kushughulikia ukamilishaji wa kituo cha afya cha Ndedo, ili wakazi wa kata hiyo waweze kupata huduma bora za afya .Kadhalika Mhe. Papian ameahidi kusimamia kuhakikisha kwamba mabweni yanayojengwa katika shule ya msingi Ndedo yanakamilika mapema na kuanza kutumika.Sambamba na kuendelea kushughulikia tatizo la maji, il kata ya Ndedo ipate bwawa la maji kwa ajili ya wakazi wa eneo hilo na mifugo yao.
Mhe. Papian pia amewataka wakazi wa Ndedo kuchangia ujenzi kwa ajili ya kidato cha tano na cha sita katika shule ya sekondari ya Ndedo.Hapa Mhe. Papian anasema” Tunataka kuanzisha kidato cha tano na cha sita hapa, tarafa yetu hii haina “A – Level”, changeni fedha tujenge.Wazee watoe madume,mwenye mbuzi atoe ,mwenye mahindi atoe, mwenye alizeti atoe, mpeleke mnadani muuze kwa ajili ya ujenzi. Na mimi nitapambana huko kwa waziri, hela zipatikane tukamilishe ujenzi”.
Katika mkutano huo wakazi wa kijiji cha Ndedo wamewasilisha kero mbalimbali kwa mhe. mbunge .Kero hizo ni ukosefu wa maji,ambapo wananchi hao wametaka kupelekewa huduma ya maji katika kijiji chao .Baadhi ya wakazi wa eneo hilo kutokupewa viwanja kwa ajili ya kujenga makazi pamoja na maeneo ya kilimo , ambapo wakazi hao wametaka kujua kwamba ni lini kero hiyo itatatuliwa.
Kero nyingine ni mgogoro kati ya hifadhi ya Mkungunero na vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo ,ambapo wanakijiji hao wameonyesha kusikitishwa na vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa wananchi katika maeneo yao na kumuomba Mhe. Mbunge kulitafutia ufumbuzi wa kudumu suala hilo, ili damu isiendelee kumwagika.Kero nyingine ni kutokuwepo kwa alama za barabarani jambo ambalo wamedai kwamba linahatarisha usalama wa wao, hususani kwa watoto.
Akijibu kuhusu kero hizo Mhe Papian amesema kwamba migogoro ipo katika maeneo mengi ya wilaya ya Kiteto, na kwamba migogoro hiyo inashughulikiwa kwa awamu, haiwezi kwisha kwa siku moja, lakini wanaendelea kuishughulikia kwa lengo la kuimaliza, na kwamba amekwishaanza kushughulikia mgogoro wa Mkungunero na kwamba ana imani kuwa kwa kushirikiana na viongozi wengine wa wilaya,mkoa na taifa mgogoro huo utamalizwa.
Kuhusu suala maji Mhe. Papian amesema kwamba maji ni miongoni mwa vipaumbele vyake ,na kwamba yeye kwa kushirikiana na viongozi wengine wa wilaya wanapamba kuhakikisha kwamba ifikapo 2020 kata hiyo inakuwa na bwawa la maji.
Kwa upande wa kero ya viwanja na mashamba ,Mhe Papian amemtaka mwenyekiti wa kijiji hicho kwa kushirikiana na Mhe. diwani pamoja na serikali ya kijiji kuhakikisha kwamba wanamaliza kero hiyo mapema iwezekanavyo kwa kuwapatia wanakijiji hao maeneo kwa ajili ya makazi na kilimo bila kubagua, bali kwa kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi waliyojiwekea katika kijiji chao.
........... MWISHO...............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa