Mapema wiki hii Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mheshimiwa Remidius Mwema amekutana na kufanya mazungumzo na Anna Walkowiak - Mwanzilishi & Mwenyekiti wa Bodi ya “Africa Help Foundation” akiambatana na Anna Paczkowska - Daktari Bingwa wa Uzazi na Magonjwa ya Wanawake (Obstetrician - Gynecologist) kupitia mradi wao unaotekelezwa Wilayani Kiteto.
Africa Help Foundation ni wadau wa maendeleo kutoka POLAND, ambao wanatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Zahanati na Jengo maalum la kujifungulia wajawazito (Marternity Home) katika Kijiji cha Ndotoi, Kata ya Laiseri Tarafa ya Sunya.
Mradi huu unalenga kutoa huduma za afya hususani Afya ya Uzazi na Mtoto kwa jamii ya wafugaji na wananchi wote katika kijiji hicho ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.
Aidha, mradi huo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali, kuhimiza jamii kuacha kujifungulia nyumbani na kwa wakunga wa jadi na badala yake jamii kuhamasishwa kutumia kituo hicho kupata huduma za afya pamoja na Elimu ya Afya kutoka kwa wataalam wanaoishi nao katika kijiji cha Ndotoi.
Mradi huu unatarajia kukamilika Januari ,2025 na wananchi wa Ndotoi wameupokea kwa mwitikio chanya.
Hata hivyo, taasisi hiyo inakusudia kushirikiana na Serikali kuongeza huduma ya uchunguzi wa vipimo mbalimbali kwa kujenga jengo la maabara.
Matarajio ya baadae ni kupandisha hadhi Kituo hiki kuwa kituo kamili cha Afya kwa kuongeza majengo ya Mama na Mtoto, chumba cha Upasuaji ili Huduma za upasuaji wa dharura na wa kupangwa kwa wajawazito wasioweza kujifungua kawaida ziweze kutolewa.
Ushirikiano baina ya Poland (Africa Help Foundation) na Serikali ya Tanzania unalenga pia nyanja za kujengeana uwezo Wataalamu wa Afya kwa mafunzo (Training) na kubadilishana Wataalam/Watumishi (Staffs Exchange) kwa kutembeleana Muda flani katika nchi hizi mbili.
Serikali itaendelea Kupeleka Watumishi,Madawa,Vitendanishi,Vifaa na vifaa tiba na kukisimamia kituo kwa uendelevu kwa kuzingatia miongozo ya Wizara ya Afya hapa nchini ili kituo hiki kiweze kutoa huduma bora za Afya kwa Wananchi wa Ndotoi.
Aidha, Serikali inatambua, inathamini na kuheshimu mahusiano mema na Wadau wote wa Maendeleo ikiwa ni pamoja na Africa Help Foundation.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa