Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian akizungumza na wakazi wa kijiji cha Irikiushibor katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Irikiushibor mwishoni mwa wiki.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Madukani akifungua Mkutano wa hadhara kwa niaba ya mwenyekiti wa kijiji cha Irikiushor. Mkutano huo umefanyika kijijini Irikiushibor mwishoni mwa wiki.
Wakazi wa kijiji cha Irikiushibor wakiwa wamekusanyika kumsikiliza mbunge wao Mhe . Emmanuel Papian kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho mwishoni mwa wiki.
Wakazi wa kijiji cha Irikiushibor wakiwasilisha kero kwa Mbunge wao Mhe. Papian kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho mwishoni mwa wiki.
............HABARI KAMILI..................
Mbunge wa jimbo la Kiteto Mheshimiwa Emmanuel Papian amewataka wakazi wa kijiji cha Irikiushbor kuamini zaidi katika mazungumzo kama njia sahihi ya kumaliza mgogoro kati yao na hifadhi ya Mkungunero, badala ya kutumia nguvu. Mhe. Papian ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Irikiushibor mwishoni mwa wiki.
Akizungumza katika mkutano huo Mhe. Papian amewasihi wanakijiji hao kuendelea kuwa watulivu wakati suala hilo linashughulikiwa.Hapa Mhe. Papian anasema “Poleni sana na matatizo yaliyowapata kutokana na hifadhi ya Mkungunero. Najua kabisa kwamba mmeumia sana na mmeghadhibika sana, lakini hili tunakwenda nalo polepole. Ninachoomba, sisi tutulie ,tuwe na imani kuwa suala hili linashughulikiwa .Nina uhakika kwamba tukienda nalo polepole tutafika mahali jambo hili litakwisha huku wote tukiwa salama”.
Aidha Mhe Papian amewahakikishia wanakijiji hao kwamba mgogoro kati yao na Mkungunero utamalizwa na watakaa kwa usalama na amani. Akieleza jitihada zinazoendelea katika kutatua mgogoro huo.Mhe. Papian amesema “ Katika mkutano wetu wa Halmashauri kuu mwezi wa tatu tulijadili kuhusu suala hili, na tunaendelea nalo.Tumeshaonana na Mhe. Kigwangala mara kadhaa, tumezungumza, sasa tunakwenda kwenye ramani. Ninaamini kwamba kwa kukaa mezani tutapata mwafaka mzuri.Tunaendelea kushirikiana na mkuu wa mkoa , nawahakikishia kwamba jambo hili tutalimaliza”.
Kadhalika Mhe Papiani amebainisha mikakati waliyonayo sasa katika kushughulikia mgogoro huo. Mhe Papian amesema “ Tuna mikakati mizuri ,kuweka mazingira mazuri kuwaokoa watu wetu ili muweze kukaa kwa amani.Tutakutana tena na Mhe. Kigwangala, tutazungumza nae ili tuone ni kwa namna gani suala hili linafika mahali linakaa sawasawa, tutakaa mezani ,tukishindwana na waziri tutakwenda kwa waziri Mkuu, kuhakikikisha kwamba jambo hili linafika mwisho”.
Nao wakazi wa kijiji cha Irikiushibor wamesema kwamba ,kwa jinsi ambavyo mbunge wao amezungumza nao kuhusiana na mgogoro huo ,wana imani nae, hivyo wanamuomba kama alivyosema yeye mwenyewe, basi aende akawatetee. Kwa sababu mgogoro huo wa mpaka ni tatizo kubwa sana kwao, kwani eneo ambalo wao wanalitambua kama mpaka kati ya kijiji hicho na hifadhi, ni tofauti na ilivyo kwa upande wa uongozi wa hifadhi hiyo , jambo ambalo limekuwa likisababisha vurugu na hata kupigwa risasi, wakati wakichunga katika eneo ambalo wao wanasadiki kama ni eneo la kijiji chao,huku upande wahifadhi wakidai kwamba ni eneo la hifadhi.Wanakiji hao wamedai kwamba wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili vya kila namna pamoja na kuchukuliwa mifugo yao, ambapo hadi sasa ng’ombe 264 za mwanakijiji mwenzao zimechukuliwa, na zimezuiwa katika eneo la ofisi za hifadhi hiyo.
Katika hatua nyingine Mhe. Papia amezungumzia suala la elimu. Mhe. Papian amesema “Hapa kuna upungufu wa vyumba vya madarasa , pana upunguvu wa walimu. Afisa mipango ichukue hiyo changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa ,tuingize kwenye mpango wetu wa maendeleo ,pesa yetu ya mfuko wa jimbo ikiingia tuchomoe tuchomeke hapo, tumalize hili tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa. Kuhusu Suala la walimu nitazungumza na Mkurugenzi ili kuhakikisha kwamba katika walimu watakao ajiriwa msimu ujao,wanapatikana walimu watakaopangwa kuja kufundisha katika shule yetu ya Irikiushibor”.
Wakati huo huo Mhe Papian amemtaka Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Irikiushibor Mwalimu Charles Mnyutwa kueleza sababu za shule hiyo kuwa ya mwisho katika matokeo ya mitihani.Ambapo mwalimu huyo amebainisha changamoto zinazowakabili katika shule hiyo, ikiwemo upungufu wa walimu, uhaba wa vyumba vya madarasa, umbali wa maeneo watoto wanakotoka hadi kufika shule ,pamoja na utoro.
Mnyutwa amesema kwamba, kutokana na umbali wanafunzi wamekuwa wakifika shule saa tatu asubuhi, na hao wanaofika saa tatu ni wachache, na kwamba wanafunzi wanakuwa wengi kuanzia saa sita mchana, hali ya kuwa vipindi vinaanza saa mbili kamili asubuhi. Na kwamba walimu wanakuwa wako tayari kuanza vipindi saa mbili, lakini katika muda huo wanafunzi wengi wanakuwa hawajafika shule, na hivyo kukosa vipindi vya asubuhi . Vilevile wanafunzi wengi ni watoro. Mnyutwa amesisitiza kwamba changamoto hizo mbili (utoro na umbali) ndizo hasa zinazosababisha shule hiyo kufanya vibaya katika matokeo ya mitihani.
Akijibu kuhusu changamoto hizo , Mhe.Papian amewata wakazi wa kijiji hicho kuhakikisha kwamba watoto wao wanakwenda shule, na sio kwenda tu,bali wawahi kufika shule ,wahudhurie vipindi vyote ili wawe na maendeleo mazuri kitaaluma.Na kwamba atafika kijijini hapo wakati mwingine kwa ajili ya kukutana na wazazi pamoja na walimu wa shule hiyo, ili wajadiliane na wapate ufumbuzi wa changamoto hizo.
Mhe Papian ametembelea kijiji cha Irikiushibor , ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku saba katika jimbo lake kukagua shughuli za maendeleo ,sambamba na kuzungumza na wapiga kura wake ili kusikia kero na changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.
............MWISHO.................
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa