Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe Tumaini Magessa akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Chekanao,kata ya kiperesa, wilayani Kiteto.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe Tumaini Magessa akisaini Kitabu cha wageni kabla ya kuanza kuhutubia mkutano.
Mwenyekiti wa kijiji cha Chekanao akifungua mkutano.
Diwani wa kata ya Kiperesa Mhe Habib Kiberenge akisalimia mkutano.
Kaimu Katibu Tawala (W) akimkaribisha Mh. Mkuu wa wilaya kuzungumza katika mkutano huo.
Afisa Ardhi (W) Ndg. Damas Gulisha akizungumza katika mkutano huo
Kaimu Afisa kilimo na ushirika (W) Ndg. Antony Kwilasa akizungumza katika mkutano huo
Wakazi wa kijiji cha Chekanao wakiwa wamekusanyika kumsikiliza Mhe. Mkuu wa wilaya .
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Chekanao wakiwasilisha kero zao kwa Mhe. Mkuu wa wilaya.
.......HABARI KAMILI......
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa amewataka wakazi wa kijiji cha Chekanao kuacha migogoro, na badala yake wajikite zaidi katika shughuli za uzalishaji mali ili waweze kupata maendeleo. Mhe. Magessa ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Chekanao ,kata ya Kiperesa , wilaya ya Kiteto jana mchana.
Akizungumza katika mkutano huo Mhe. Magessa amesema” Haya mambo ya migogoro isiyokwisha yanatuchelewesha kupata maendeleo. Kama mkuu wa wilaya sasa, mpango wangu ni kujikita katika kutafuta masoko, kwa sababu watu wanalima sana, na bei ya mazao ndani ya wilaya yetu iko chini sana. Nahitaji kushughulika kuhakikisha masoko yanapatikana katika mikoa mingine, na hata nje ya nchi, ili mazao yetu yauzwe kwa bei nzuri itakayo wanufaisha wakulima na kuwawezesha kujiendeleza kiuchumi. Lakini hilo halitawezekana kama migogoro ikiendelea. Kwa sababu tutabaki kila siku kukimbizana na matatizo ambayo ni matokeo ya migogoro, tunatumia muda mwingi kushughulikia migogoro, badala ya kufikiria jinsi ambavyo tutainua uchumi wetu ”.
Aidha Mhe. Magessa ameitaka serikali ya kijiji kuitisha mkutano mkuu wa kijiji ili kupanga matumizi bora ya ardhi ya kijiji , kama njia ya kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji , ambapo watakaa na kupanga na kukubaliana kutenga maeneo ya mifugo, maeneo ya kilimo, maeneo ya makazi na maeneo ya hifadhi .
Akisisitiza kuhusu kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya kijiji hicho, Mhe Magessa amesema “Hatuwezi kutenganisha kilimo na ufugaji, ni lazima mfanye maamuzi, mkubaliane kwamba ni maeneo gani mnalima,maeneo gani mnafuga.Na mkishakubaliana, kama wewe ulikuwa unalima eneo ambalo ni la mifugo ukubali kuondoka uende eneo la kilimo,kama ulikuwa unafuga eneo ambalo ni la kilimo, ukubali kuondoka uende eneo la mifugo. Baada ya kuweka mpango huo na kukubaliana ,wataalamu hawa watakuja kurasimisha. Hiyo ndiyo itakuwa salama ya kijiji, vinginevyo itakuwa ni ngumi mkononi, migogoro haiwezi kwisha”.
Kadhalika Mhe Magessa amewashauri wakazi wa kijiji hicho kubadilika, na kuachana na kilimo na ufugaji wa mazoea,ambao hauna tija,badala yake walime kilimo chenye tija na kufuga kwa tija, ambapo watakuwa wakiwatumia wataalamu wa kilimo na mifugo kulima na kufuga kwa kufuata kanuni za kilimo na ufugaji bora. Kwa kufanya hivyo wataweza kulima mashamba madogo na kuvuna mavuno mengi, sambamba na kufuga mifugo michache ambayo itakuwa na ubora unaotakiwa, itatoa maziwa mengi , na vilevile itauzwa kwa bei nzuri. Hivyo kupata muda wa kufanya shughuli nyingine za kiuchumi na za kijamii, vilevile kutapunguza tatizo la ukosefu wa ardhi, kwani hata wale ambao hawana maeneo ya kulima, watapata , kwa sababu watu hawatahitaji maeneo makubwa sana kwa ajili ya shughuli za kilimo ,na mifugo itakuwa michache , itafugwa kwa utaratibu ,haitahitaji maeneo makubwa sana ya malisho kama ilivyo sasa,ambapo wingi wa mifugo ni moja wapo ya sababu migogoro kati ya wakulima na wafugaji, ambapo kutokana na uhitaji wa eneo kubwa la malisho, baadhi ya wafugaji huingiza mifugo katika mashamba ya wakulima ili kulisha mifugo yao.
Katika hatua nyingine Mhe. Magessa amezungumzia suala la elimu, ambapo amewataka wazazi na walezi kuhakikisha kwamba watoto wote ambao wamefikia umri wa kwenda shule, wanakwenda shule,na wale ambao umri wao umesogea na hawajapelekwa shule waandikishwe katika Mpango wa Elimu kwa Walioikosa(MEMKWA) ili asiwepo mtu ambaye atakosa elimu.Mhe. Magessa amesisitiza kwamba suala la kuwapeleka watoto shule ni suala la lazima, na wala sio suala la hiyari.
Katika mkutano huo wanakijiji wa Chekanao wamewasilisha kero zao kwa Mhe. Mkuu wa wilaya ambapo kero kubwa ni kutokukamilika kwa mradi wa maji kwa muda mrefu jambo ambalo linasababisha wanakijiji hao kuendelea kukosa kukosa maji, ilhali wano mradi wa maji katika kijiji chao. Kero nyingine ni wafugaji kuchungia kwenye mashamba ya wakulima, na mgogoro wa bwawa kwa wakazi wa kitongoji cha Kichwa cha tembo ,ambapo wanadai kwamba wafugaji wanaingiza mifugo na kuchafua maji katika bwawa ambalo ndilo linalotumiwa na wakazi kitongoji hicho kwa matumizi ya binadamu.
Mhe. Magessa ametoa majibu kwa baadhi ya kero , vilevile ameahidi kufanyia kazi kero zote zilizowasilishwa katika mkutano hou.Sambamba na kufanya mkutano mwingine katika kijiji hicho ndani ya mwezi huu wa kumi kwa ajili ya kutoa majibu ya kero hizo ambazo hazijatolewa majibu,kufuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa , pamoja na kuzungumza na wanakijiji hao.
.......... MWISHO...........
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa