Katika hatua inayoonesha dhamira ya serikali kuboresha mazingira ya elimu nchini, Shule ya Msingi Umoja iliyopo katika kata ya Matui, wilayani Kiteto, imepokea kiasi cha shilingi milioni 182.7 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule hiyo.
Fedha hizo ni sehemu ya juhudi za serikali kupitia programu ya BOOST, zitatumika kujenga vyumba vinne vya madarasa na matundu sita ya vyoo kwa ajili ya elimu ya msingi. Aidha, mradi huo unahusisha pia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya mfano ya awali pamoja na matundu sita ya vyoo mahsusi kwa wanafunzi wa elimu ya awali.
Akizungumza siku ya Julai 23, 2025 shuleni hapo wakati wa kuutambulisha mradi huo kwa serikali ya Kijiji, Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Mwl. Elizabeth Mlaponi, amesema kwamba mradi huo utaleta mageuzi makubwa katika mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
"Mradi huu sio tu utaongeza nafasi ya kujifunza, bali pia utaongeza hamasa kwa wanafunzi kuhudhuria masomo kwa sababu sasa watakuwa katika mazingira rafiki na salama," alisema Mwl. Mlaponi.
Kukamilika kwa miundombinu hiyo kutabadili kabisa sura ya Shule ya Msingi Umoja na kuwa chachu ya kuinua kiwango cha elimu, hasa kwa watoto wenye umri mdogo wanaoanza safari yao ya kielimu.
Mradi huu ni ushahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuwekeza kwa vitendo katika sekta ya elimu, ili kuhakikisha kila mtoto anapata fursa sawa ya kusoma katika mazingira bora, salama na yenye kuhamasisha mafanikio ya kitaaluma.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa