Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Emmanuel Papian,Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Lairumbe Mollel , Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ndugu Tamim Kambona , Kamati ya Ulinzi na usalama, viongozi wa kijiji ( Waliokaa kwenye viti) pamoja na wakazi wa kijiji cha Kimana kata ya Partimbo wilayani Kiteto wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti alipokuwa akizungumza na wakazi hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.
Wakazi wa kijiji cha Kimana kata ya Partimbo wilayani Kiteto wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti alipokuwa akizungumza nao katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.
.......HABARI KAMILI......
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Aagiza Kuvunjwa kwa Makazi holela Wilayani Kiteto
Mkuu wa mkoa wa Manyara Mheshimiwa Alexander Mnyeti ameagiza kuvunywa kwa makazi holela yaliyojengwa katika kata ya Partimbo.Na wamiliki wa makazi hayo kuhamia katika kijiji cha Kimana,ambacho ni kijiji halali . Mhe. Mnyeti ametoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kimana kilichopo kata ya Partimbo wilayani Kiteto.
Akizungumza wakati anatoa agizo hilo Mhe. Mnyeti anasema “Mkuu wa wilaya nakuagiza, hakikisha unasafisha barabara yote, kote kwenye makazi holela.warudishe hapa,wakae hapa,na mji huu utakuwa mkubwa sana.Maana taarifa niliyonayo nimeambiwa wako watu hapa wanasubiri msimu wa kilimo wanakuja kulima na kuondoka.Kama huwezi kuishi nenda kwenu kaishi. Manyara sio sehemu ya kuchezea,Mnakuja kulima,baada ya mavuno mnawaachia watu takataka mnaondoka.Nataka nijue kama hiki ni kijiji,kitongoji au ni kitu gani.Nataka nikirudi hapa nikute watu wote wamehamia kwenye kijiji hiki, na ulinzi na usalama uimarishwe na watu waishi kwa amani”.
Mheshimiwa Mnyeti pia amemtaka Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mheshimiwa Tumaini Magessa kusimamia kazi hiyo ya uvunjaji wa makazi holela ,na ametoa mwezi mmoja kukamilika kwa kazi hiyo, ambapo amemtaka Mhe. Magessa kumpa taarifa ya namna alivyotekeleza maagizo hayo,mara baada ya muda huo .
Katika hatua nyingine Mhe. Mnyeti amewapongeza wakazi wa kijiji cha Kimana kwa kuheshimu mpango wa matumizi bora ya ardhi .Wakati huo huo ametoa onyo kali kwa wakazi wa kijiji hicho ambao hawaheshimu mpango wa matumizi bora ya ardhi na wavamizi wa mashamba ya watu kwamba waache mara moja kulima kwenye maeneo ambayo sio mashamba, kwani kufanya hivyo ni kuchochea migogoro . Mhe. Mnyeti anasema “Ukianzisha shamba jipya ambalo haliko kwenye utaratibu unatafuta ugomvi.Hatutaki kugombana.Mnapaswa mkalime kwenye maeneo ambayo mmekubaliana. Na waliovamia mashamba yasiyo ya kwao waondoke mara moja”.Mheshimiwa Mnyeti amewaambia wananchi hao kwamba wasiende kulima mashamba ambayo hawajui wamiliki wake.na ambayo hawajui wameyapataje kwani kufanya hivyo ndiko kunakosababisha migogoro.Hapa Mhe. Mnyeti anasema ‘‘Unakwenda kwenye shamba ambalo mwenyewe humjui, unaingiza trekta unalima.mwenyewe akija kesho mnapigana mikuki. Sasa hao wanaosababisha chokochoko sitaki kusikia habari hii tena”.
Kata ya Partimbo ndio kata ambayo eneo lake kubwa limevamiwa na watu na kujengwa makazi holela.Makazi hayo ambayo yako nje ya utaratibu yanasababisha wakazi wa maeneo hayo kukosa huduma muhimu kama shule, zahanati ,maji na umeme.
................. MWISHO................
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa