Katika juhudi za kuboresha ufanisi wa kukabiliana na maafa Katika Halmashauri ya Wilaya Kiteto, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, ilifanya kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo kuanzia Oktoba 28-30,2024 wilayani hapo ili kuandaa mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa. Kikao hiki kiliongozwa na wataalamu kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na wataalamu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Mratibu wa Maafa wa Mkoa wa Manyara. Mbali na wataalumu hao kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji, kikao kazi hicho kilihudhuriwa na wakuu wa taasisi zote wilayani hapa pamoja na wadau mbalimbali.
Katika kikao hicho, washiriki wa kikao hicho walijadili kwa kina mfumo na miongozo ya usimamizi wa maafa, wakilenga kuboresha mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kutokea katika wilaya. Mada nyingine zilizozungumziwa ni pamoja na tathmini ya maafa katika halmashauri, ambayo itasaidia kutambua hatari na athari zinazoweza kuikabili jamii.
Aidha washiriki hao walijadili mgawanyo wa majukumu katika mpango wa kukabiliana na maafa, ili kuhakikisha kuwa kila taasisi inajua jukumu lake na inashirikiana kwa ufanisi katika kukabiliana na maafa. Aidha, kikao kilijikita pia katika kutathmini uwezo wa wilaya wa kukabiliana na maafa, ikiwa ni pamoja na rasilimali zilizopo na mahitaji ya kuongeza nguvu katika eneo hili.
Kikao hiki ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za serikali katika kuimarisha usimamizi wa maafa na kuhakikisha kwamba jamii inakuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maafa. Wataalamu walisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na jamii katika kuhakikisha kuwa mipango inayoundwa inatekelezwa kwa ufanisi.
Kikao kilihitimishwa kwa makubaliano ya kuandaa mpango mkakati ambao utawasaidia wakazi wa Kiteto kuwa na maandalizi mazuri ya kukabiliana na maafa, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendelea na mafunzo na elimu kuhusu usalama wa jamii.
Kwa ujumla, kikao hiki kinaashiria hatua muhimu katika kujenga uwezo wa halmashauri ya Kiteto katika usimamizi wa maafa, na kuonyesha dhamira ya serikali katika kulinda maisha na mali ya wananchi.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa