Naibu Waziri wa OR- TAMISEMI Mhe. Mwita M. Waitara akizunguza katika kikao chake na watumishi kilichofanyika ndani ya ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto mapema leo.Waliokaa upande wa kulia ni mwenyekiti wa halmashauri Mhe. Lairumbe Mollel na upande wa kushoto ni kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Ndg. Christopher Simwimba.
Katibu Tawala Ndg. Musa Waziri akimkaribisha Naibu waziri kuzungumza na watumishi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto Ndg. Christopher Simwimba akitoa akitambulisha watumishi.
............HABARI KAMILI..................
Naibu waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) Mheshimiwa Mwita Waitara amewataka watumishi kuwajibika katika nafasi zao.Mheshimiwa Waitara ameyasema hayo wakati wa kikao chake na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto kilichofanyika mapema leo tarehe 15.12.2018 katika ukumbi wa Halmashauri .
Akizungumza katika kikao hicho Mheshimiwa Waitara amewaasa watumishi kuhusu kufanya kazi kwa bidii ,sambamba na kufuata taratibu ,hapa Mhe. Waitara anasema “ Wito wangu kwenu watumishi, kila mtu awajibike kwenye nafasi yake.Serikali inataka watumishi wafanye kazi .Msifanye siasa kazini.Acheni maneno maneno.Usicheze ngoma ambayo sio ya kwako,suala la utumishi ni suala binafsi.Mtu hata kama amelipwa jana,akigundua kama unataka kumkopa atakwambia sina hela.Kila mtu ana namba yake ya ajira.Kama una madai au malalamiko, kuna taratibu za kufuata. Sio sawasawa kufanya kazi chini ya kiwango kwa sababu una madai”.
Mheshimiwa Waitara amesema kwamba kupandishwa vyeo, kuna vigezo. Na kwamba wao kama serikali wanafahamu kwamba idara nyingi zina malamiko , hususani idara ya elimu , walimu wanalalamika kwamba hawapandishwi madaraja, lakini pia wanafahamu kwamba kuna watumishi hawatimizi wajibu wao, hawafanyi kazi. Lakini pia wanafahamu kwamba wako watumishi wazuri sana Halmashauri lakini hawapandishwi madaraja kwa sababu kuna watu wanawafanyia wenzao roho mbaya, taarifa hazikamiliki,kwa hiyo mtumishi anakaa anasubiri kupandishwa cheo, lakini hapandishwi cheo.
Kadhalika Mhe. Waitara amesema kwamba wameelekeza wakuu wa idara kuwa wajipangie ratiba,kupunguza umbali , wafike ofisi za kata wakawasikilize watumishi walioko huko ,wasisubiri watumishi hao wawafuate. Kadhalika amewataka wakuu hao wa idara kuwa wabunifu katika kushughulikia masuala mbalimbali katika idara zao,wawe watatua matatizo, wasiwe wa kulalamika kama watumishi walio chini yao, watatue matatizo, yale yatakayokuwa yanawashinda ndio wayapelekwe kwa Mkurugenzi na kutokea kwa Mkurugenzi yatafika katika ngazi nyingine za juu kwa utatuzi.
Mheshimiwa Waitara pia amezungumzia kuhusu lugha ambazo zinatumika kwa watumishi ,ambapo amesema kwamba kuna Halmashauri nyingine maafisa utumishi wana lugha ambazo sio nzuri kwa watumishi.Amesema kwamba kama wanaona watumishi wanazungumza au kufanya mambo ambayo sio sahihi , kazi yao ni kuwaelewesha kwa sababu wao wanaelewa zaidi kuliko watumishi wengine.
Aidha Mheshimiwa Waitara ametoa maelekezo kuhusu watumishi wa idara ya afya kulipwa shilingi 120,000/= kila mwaka kwa ajili ya sare za kazi.Amesisitiza kwamba maelekezo hayo yametokana na agizo la Waziri Mkuu Mhe Kasim Majaliwa ambaye ameagiza kuwa kabla ya mwaka 2018 kwisha watumishi hao wawe wamelipwa fedha hizo ambazo ni kutoka katika mapato ya ndani ya Halmashauri.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Waitara ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Kiteto kwa ukusanyaji mzuri wa mapato ,ambapo amesema kwamba katika mkoa wa Manyara ,wilaya ya Kiteto ndiyo inaongoza . Vile vile ameipongeza kwa kiwango kizuri cha ufaulu ambapo amesema kwamba pamoja na kuwa wilaya ni ya wafugaji, lakini inafanya vizuri kwenye elimu,jambo ambalo ni la kupongezwa sana.
Katika kikao hicho Mhe Waitara amezungumzia kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo maadili ya utumishi wa umma, ushirikiano kati ya watumishi na wakuu wa idara, utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya serikali,utii wa sheria na kanuni za nchi, pamoja na wajibu wa viongozi katika utatuzi wa migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
............MWISHO..............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa