Kata ya Ndirigishi imepokea Cheti cha Pongezi kwa kuibuka kinara katika kutekeleza Mkataba wa Lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto katika mwaka 2023/2024.
Cheti hicho cha Pongezi ambacho kilikabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhe.Remidius Mwema, kimetolewa katika kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa Robo ya Nne ya mwaka 2023/2024 kilichofanyika Agosti 1,2024 katika Ukumbi wa Halmashauri.
Afisa Lishe (W), Beatrice Lutanjuka, amesema kwamba Kata ya Ndirigishi imepongezwa kwa jitihada kubwa wanayofanya ambapo wanafunzi wote 2,200 kutoka shule nne za msingi na moja ya sekondari katika kata hiyo wanakula chakula shuleni.
Mara baada ya kupokea Cheti hicho cha Pongezi, Mhe. Mwema alimtaka Mtendaji wa kata hiyo Ndg. Robert Augustino Meikasi kueleza siri ya mafanikio hayo. Akijibu swali la Mkuu wa Wilaya, Ndg Meikasi amesema kwamba katika kata yake chakula kinatolewa kwa wanafunzi wote hata wale ambao wazazi wao hawajachanga chakula.
“Kwenye kata yangu hata wanafunzi ambao wazazi wao hawajachanga chakula, tunawapa chakula huku tukiendelea kuwafuatilia kwa karibu wazazi ambao hawajachanga ili waweze kuchanga maana watoto wao wanakua tayari wameshaanza kula chakula shuleni”, ameongeza Meikasi.
Aidha, Mhe. Mwema amewataka watendaji kutoka kata zote 23 za wilayani hapo, kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa Mkataba wa Lishe katika kata zao kwani hayupo tayari wilaya yake kuwa wa mwisho kwenye utekelezaji wa mkataba huo ukizingatia Wilaya ya Kiteto inazalisha chakula kwa wingi.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa