Mlengwa wa TASAF bibi Mariamu Kombo Mbaruku akiwa na watoto wake nje ya nyumba yao. Nyumba hii ilikuwa ni chumba kimoja tu ,lakini Mama huyu aliweza kuongeza chumba kingine kimoja kwa kutumia fedha za ruzuku za PSSN na kufanya nyumba hii kuwa ya vyumba viwili kama inavyoonekana sasa.
.........HABARI KAMILI.......
‘‘Nimeboresha Makazi yangu kwa Fedha za PSSN’’ Mlengwa wa TASAF Wilayani Kiteto
Mlengwa wa TASAF bibi Mariamu Kombo Mbaruku amesema kwamba TASAF kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (PSSN) imemuwezesha kuboresha makazi yake. Bibi Mariamu ameyasema hayo nyumbani kwake ,katika kijiji cha Bwagamoyo wilayani Kiteto wakati alipotembelewa na Afisa Ufuatiliaji wa TASAF ndugu Kishari Shegella ambapo amesema kwamba kwa kutumia fedha za PSSN ameweza kuongeza chumba kimoja katika nyumba yake .
Akizungumza na ndugu Shegella bibi Mariamu amesema kwamba kabla ya kuingia katika PSSN alikuwa akiishi kwenye chumba kimoja, lakini baada ya kuanza kupokea fedha za PSSN ameweza kujenga chumba kingine.Hapa Bibi Mariam anafafanua zaidi anasema ‘‘Kabla sijaanza kupokea ruzuku ya TASAF nilikuwa na chumba kimoja, ambacho ndicho nilikuwa naishi na watoto wangu wote watano, lakini naishukuru TASAF kwani kwa kutumia fedha za PSSN nimeweza kuboresha makazi yangu kwa kujenga chumba kingine . Nimeongeza chumba kingine ambacho nimejenga kwa matofali na nimepaua kwa mabati’’.
Kadhalika bibi Mariamu amesema kwamba baada ya kuanza kupokea fedha za PSSN alianzisha biashara ya kuuza mboga za majani,ambapo alitumia shilingi 15,000 kama mtaji anzia wa biashara hiyo, na inampatia faida isiyopungua shilingi 2000 kila siku , fedha ambayo inamsaidia kununua chakula . Bibi Mariamu ambaye ndiye mkuu wa kaya kwa sasa baada ya kufiwa na mumewe , kaya ambayo ina jumla ya wanakaya 6 anasema, ‘‘ hali ya chakula nyumbani kwangu ilikuwa ngumu sana, mimi na familia yangu tulikuwa tunakula milo miwili tu kwa siku. Asubuhi tunakunywa uji na usiku tunakula ugali, mchana tulikuwa hatuli kabisa, lakini sasa hivi tunakula milo mitatu kwa siku, chai asubuhi, chakula mchana na chakula cha usiku”.
Kwa upande wa mavazi bibi Mariamu amesema kwamba PSSN inamuwezesha kupata mavazi , hususani sare za shule kwani kabla ya kuingia kwenye PSSN hakuwa na uwezo wa kununua sare za shule za watoto wake watatu ambao ni wanafunzi, wawili wakiwa shule ya msingi na mmoja sekondari jambo ambalo lilikuwa linasababisha watoto wake kwenda shule na sare zilizochakaa sana,lakini baada ya kuanza kupokea fedha za PSSN mambo yamekuwa tofauti . Bibi Mariamu anasema ‘‘ Kuna tofauti kubwa kabla ya kupata fedha za TASAF na sasa, sasa hivi watoto wangu nimeweza kuwanunulia sare mbilimbili za shule, na nguo nyingine za kuvaa ,na mimi mwenyewe naweza hata kununua kanga , tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma ambapo hali yetu kwa upande wa mavazi ilikuwa mbaya sana’’.
Aidha bibi Mariamu amesema kwamba kwa kutumia fedha za PSSN ameweza kulima shamba ekari mbili na amepanda mahindi na alizeti,ambapo kama mvua zitakuwa za kutosha anategemea kuvuna mahindi magunia kumi na alizeti magunia manne .
Sambamba na hayo bibi Mariamu ameeleza mipango yake ya baadae ya maendeleo ambapo amesema kwamba ni kuongeza biashara yake ya mbogamboga, kuanzisha mradi wa ufugaji mbuzi,kondoo na kuku pamoja na kuongeza shamba kwa kukodi ili aweze kulima shamba kubwa zaidi ya ambavyo amelima mwaka huu .Bibi Mariamu amesema kwamba anapokea fedha za PSSN shilingi 36,000 , anapozipata fedha hizo anajitahidi kuzitumia kwa uangalifu na kuweka akiba kidogo kidogo ili aweze kufikia malengo yake.
........... MWISHO.............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa