Shule ya Msingi Kurash iliyopo katika kata ya Lengatei, wilayani Kiteto, imeendelea kunufaika na programu ya BOOST baada ya kupokea mradi mpya wa ujenzi wa miundombinu ya elimu yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 153.
Kupitia mradi huo mpya, shule hiyo inatarajiwa kujenga vyumba vitano vya madarasa ya elimu msingi, matundu 11 ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi wa elimu msingi na vyoo viwili kwa ajili ya walimu. Hatua hii inalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo.
Julai 25, 2025 wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji walifika katika shule hiyo kwaajili ya kuutambulisha mradi huo kwa wananchi ikiwa ni moja ya miongozi ya utekelezaji wa mradi huo.
Hii ni mara ya pili kwa shule ya Kurash kupokea fedha kupitia programu ya BOOST ndani ya kipindi kifupi. Katika mwaka wa fedha 2024/2025, shule hiyo ilinufaika na mradi mwingine uliogharimu shilingi milioni 157.7, kwaajili ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa ya elimu msingi, vyoo matundu sita pamoja na vyumba viwili vya madarasa ya awali na matundu mengine sita ya vyoo kwa wanafunzi wa elimu hiyo ya awali.
Mradi huo wa awali tayari umekamilika na umeleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za elimu shuleni hapo, huku mradi mpya ukitarajiwa kuongeza uwezo wa shule hiyo kuhudumia idadi kubwa ya wanafunzi kwa ufanisi zaidi.
Hatua hizi ni sehemu ya jitihada za serikali kupitia programu ya BOOST katika kuinua ubora wa elimu ya awali na msingi, hasa maeneo ya vijijini, ambapo changamoto za miundombinu zimekuwa kikwazo kwa muda mrefu.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa