Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Mh. Edward Olelekaita amesema kwamba muda wowote yupo tayari kufuatilia fursa mbalimbali kwaajili ya maendeleo ya kiteto.
Haya ameyasema Septemba 12, 2023 katika Ukumbi wa Maktaba kwenye hafla fupi ya kukabidhi kompyuta mpakato kwa wakuu wa shule 13 ambapo 11 ni kutoka shule za sekondari na wawili kutoka shule za msingi.
Mh. Olelekaita alitoa rai kwa wakuu wa shule hao 13 kuzitumia kompyuta hizo kwa kuweka kumbumbuku ili waweze kuongeza ufanisi katika majukumu yao.
“Kompyuta hizi zitawanufaisha sana. Kwa sekondari zilizobaki nazo zitapatiwa kompyuta mwakani kupitia mfuko wa jimbo. Kila wakati ikitokea mkasikia kuna fursa yoyote na kokote naomba mnijulishe nami nipo tayari muda wowote kuzifuatilia, lazima Kiteto isikike vizuri”, aliongeza Mh. Olelekaita.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji (W), Bwana Erasmo Tellun Ndelwa ambaye ni Afisa Mipango (W), amemshukuru sana mbunge huyo kwa jitihada zake ambazo amekua akizifanya katika kuchochea maendeleo ya Kiteto. Aliongeza kwa kusema kwamba Mh. Olelekaita amekua mstari wa mbele katika kufuatilia na kuhakisha pesa zote ambazo zipo kwenye bajeti zinafika halmashauri kwa wakati.
Nae Afisa Elimu Sekondari (W), Bwana Ally Kichuri, alisema kwamba idara ya elimu msingi na sekondari inamshukuru sana Mh. Olelekaita kwakua amekua akizisaidia idara hizo katika mambo mengi ikiwemo kufuatilia na kuhakikisha Kiteto inapata shule mpya.
Mmoja ya wakuu wa shule hizo, Bwana Asheri Lowasa ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Edward Olelekaita, alimshukuru mbunge kwa niaba ya wenzake na aliongeza kwa kusema kwamba kompyuta hizo ni chachu ya kuwafanya waendelee kufanya vizuri zaidi.
Kompyuta zilizokabidhiwa zina jumla ya thamani ya shilingi 13,000,000. Mh. Olelekaita aliahidi kutoa kompyuta hizo akiwa kwenye ziara zake katika mwaka 2022/2023 maeneo mbalimbali kwenye jimbo hilo.
Shule zilizopokea kompyuta hizo ni shule za msingi Boma na Laalakiri ilhali upande wa sekondari shule zilizopokea ni Dosidosi, Kibaya, Kijungu, Edward Olelekaita, Partimbo, Dongo, Magungu, Njoro, Kiperesa na ECO.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa