Shule ya Msingi Olengashu iliyopo katika Kijiji cha Kimana, Kata ya Partimbo, imepokea jumla ya shilingi 88,600,000 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo kupitia Programu ya BOOST.
Akizungumza siku ha Julai 21, 2025 katika kikao maalum cha kutambulisha mradi huo kwa wajumbe wa serikali ya kijiji, viongozi wa chama na walimu wa shule hiyo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Awali na Msingi Wilaya ya Kiteto, Mwl. Beatus Temba, alisema kuwa kati ya fedha hizo, shilingi 75,000,000 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa, shilingi 12,600,000 kwa ujenzi wa matundu sita ya vyoo, na shilingi 1,000,000 kwa ajili ya shughuli za ufuatiliaji katika ngazi ya shule.
“Hivi tunavyoongea, tayari jumla ya fedha hizo zimeingizwa kwenye akaunti ya shule. Jukumu lenu sasa ni kuteua wajumbe wa kamati ya ujenzi na kamati ya mapokezi ya vifaa, ili wapewe mafunzo na utekelezaji wa mradi uanze mara moja,” alisema Mwl. Temba.
Mradi huu unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Olengashu, sambamba na kuhakikisha usafi na afya ya wanafunzi kupitia uboreshaji wa miundombinu ya vyoo.
Programu ya BOOST imeendelea kuwa mkombozi kwa shule mbalimbali nchini kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za elimu.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa