Bw. Sempeho Manongi ( Meneja wa SIDO mkoa wa Manyara) akitoa ufafanuzi kuhusu Mkakati wa uanzishwaji na uendelezwaji Kongano wilayani Kiteto.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mh. Tumaini Magessa akifungua warsha ya Mkakati wa Uanzishwaji na uendelezwaji Kongano iliyoandaliwa na SIDO mkoa wa Manyara.
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Bw. Rafael Makoninde akizungumza katika warsha ya Mkakati wa Uanzishwaji na uendelezwaji Kongano iliyoandaliwa na SIDO mkoa wa Manyara.
Wataalamu wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto wakisikiliza kwa makini maelekezo katika warsha ya Mkakati wa Uanzishwaji na uendelezwaji Kongano iliyoandaliwa na SIDO mkoa wa Manyara .
Habari kamili
SIDO Mkoa wa Manyara Waendesha Warsha Kuhamasisha Mkakati wa Uanzishwaji wa Viwanda kwa Kutumia Dhana ya Kongano Wilayani Kiteto.
SIDO mkoa wa Manyara wameendesha warsha ya kuhamasisha mkakati wa uanzishwaji wa viwanda vya Kongano. Warsha hiyo imefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya kiteto ikiwahusisha Mkuu wa wilaya ya Kiteto, kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto na wataalamu wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto.
Mwezeshaji katika warsha hiyo meneja wa SIDO mkoa wa Manyara bwana Sempeho Manongi amesema kwamba ili uanzishwaji viwanda kwa kutumia dhana ya uendelezaji Kongano uweze kufanikiwa katika wilaya ya Kiteto halmashauri ya wilaya inatakiwa kuainisha rasilimali zilizopo, rasilimali hizo zitumike kuanzisha viwanda vidogo. Hata hivyo bwana Manongi amesema kwamba ili rasilimali hizo ziweze kuwa fursa na wajasiliamali waweze kuzitumia kuanzisha viwanda, ni lazima halmashauri iweke mazingira wezeshi ambapo uanzishwaji na uendelezwaji wa kongano za viwanda utawezekana. Halmashauri zinatakiwa kutenga maeneo ya kutosha , pia kwa kutumia wataalamu wake, halmashauri ifanye juhudi katika kujenga uelewa kwa wananchi, hii ikiwa ni pamoja na uwasilishwaji wa mkakati wa SIDO na uundwaji wa kamati ya wilaya ambayo itakuwa mahususi kwa ajili ya kuwaunganisha walengwa wa Kongano na wataalamu wilayani Kiteto.
Serikali ya awamu ya tano imeweka msisitizo katika kuhamasisha uanzishwaji na uendelezwaji wa viwanda.Wadau muhimu ; wazalishaji wa malighafi, wasambazaji, wafanyabiashara, wasafirishaji, wanunuzi na wauzaji wajengewe uelewa wa dhana ya Kongano za viwanda zinazojikita katika rasilimali zilizochaguliwa wilayani ambazo zitaendelezwa kwa ushirikiano kati ya wataalamu kutoka katika halmashauri ya wilaya na wadau hao kwa kutumia dhana ya mnyororo wa thamani. Dhana ya uendelezaji Kongano haihitaji kuanza mambo mapya, rasilimali zinazopatikana katika wilaya zinatumika kama fursa za uanzishaji viwanda. SIDO kama msimamizi wa maendeleo ya viwanda vidogo vidogo Tanzania wanatoa huduma ya kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo kulingana na fursa zilizopo, wanatoa huduma ya mafunzo, huduma ya teknolojia, msaada wa masoko , na ndio wenye jukumu la kuhamasisha halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya uanzishwaji wa Kongano.
Aidha dhana ya Kongano ni muhimu sana katika uendelezaji viwanda kwani Kongano za viwanda zinasaidia katika kurahisisha mawasiliano na taarifa, kupata teknolojia, kuongeza ujuzi, kuongeza uwezo wa kuzalisha, ushirikiano, kupata masoko, kupata huduma wezeshi kirahisi kama vile huduma za kudhibiti ubora na viwango kutoka katika taasisi kama vile TBS na TFDA na pia kurahisisha uwezeshaji kupitia serikali au wahisani. Hivyo kwa kuzingatia jografia ya wilaya ya Kiteto, hususani mji wa Kibaya ambao unakua kwa kasi, pia ni njia panda ya kuelekea miji mingine kama Dodoma, Dar es Dalaam, Babati na Tanga , ni soko la wakulima na bado una fursa ya kupangwa. Uanzishwaji wa viwanda vidogo vya kusindika mazao ya kilimo na mifugo,Kuzalisha bidhaa za ngozi, kuzalisha vyuma, kuzalisha samani, matengenezo ya magari na uwekezaji katika vyuo vya ufundi, utakuwa na mafanikio makubwa sana.
“ KONGANO’’ ni mkusanyiko wa viwanda vilivyo karibu karibu vinavyofanya shughuli zinazofanana au kushabihiana vikisaidiwa na watoa huduma mbalimbali wanaolenga shughuli za kongano husika.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa