Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Remidius Mwema amewasisitiza watumishi wa ajira mpya wilayani hapa kufanya kazi kwa bidii maeneo waliyopo badala ya kutamani kufanya kazi mijini pekee.
Akizungumza Septemba 16, 2025 wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Mhe. Mwema alisema maendeleo ya kweli hayaletwi na mazingira bali na bidii ya mtu binafsi.

“Huhitaji kuwa mjini au kuwa na nafasi kubwa ili uweze kuleta maendeleo na mabadiliko ni vizuri kila moja astawi alipopandwa", alisema Mhe. Mwema.
Mhe. Mwema aliendelea kuwaasa kwamba kila mmoja atengeneze alama kwenye eneo lake la kazi kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi.
Hata hivyo Mhe. Mwema aliwataka watumishi wa wapya wajifunze vizuri mazingira yao ya kazi akieleza kua hawawezi kufanya kazi kwa ufanisi endapo hawana uelewa mzuri wa mazingira yao kazi.
Sambamba na hayo Mhe. Mwema aliwakumbusha watumishi wa ajira mpya kutambua majukumu yao, kuheshimu mipaka ya kazi na kufuata sheria, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma.
Aidha, Mhe. Mwema alisisitiza maadili na matumizi bora ya teknolojia kwa kuepuka matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
"Kesho yako ipo mikononi mwako, utaijenga wewe au utaibomoa wewe", aliongeza Mhe. Mwema.
Mafunzo hayo ya siku moja yalihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, CPA Hawa Abdul Hassan ambaye alihitimisha mafunzo ya waajiriwa wapya.
Mafunzo hayo yalitolewa kwa Watumishi wa ajira mpya kutoka Idara ya Utawala, Kilimo na Mifugo, Ununuzi na Ugavi, Biashara pamoja na Michezo na Utamaduni.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa