Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, Julai 23, 2025 ameongoza kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe katika kipindi cha Robo ya Nne (April-June 2025).
Kikao hicho kimebeba uzito wa kijamii kwa kuangazia mafanikio, changamoto na msukumo mpya katika utekelezaji wa mkataba huo.
Katika tathmini hiyo, kata ya Sunya imeshika nafasi ya kwanza kwa kuonesha viwango vya juu vya utekelezaji wa afua za lishe, ikifuatiwa na Ndirigishi na Njoro. Kata hizi tatu zimepongezwa rasmi na kupewa vyeti vya kutambua juhudi zao katika kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni katika mwaka 2024/25.
Aidha, kata ya Magungu ilitajwa na kupongezwa kwa kuonyesha ongezeko la ufanisi licha ya kuwa haikuingia katika tatu bora. Hii ni dalili kwamba juhudi za kimkakati zinaanza kuzaa matunda hata kwa kata ambazo awali zilikuwa nyuma.
Kwa upande mwingine, kata ya Lengatei ilitajwa kama iliyofanya vibaya katika robo hiyo ya nne na hivyo kukabidhiwa bendera nyeusi.
Mhe. Mwema ametoa msisitizo mzito kwa watendaji wa kata kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa mkataba wa lishe, huku akiwataka kuhakikisha wanafunzi wote wanapata angalau mlo mmoja shuleni kila siku.
Vilevile amehimiza wazazi na walezi kushiriki kikamilifu katika mchakato huo kwa kutoa mchango wa chakula cha wanafunzi.
"Tafsiri ni fupi, kile chakula ambacho angekula mtoto nyumbani unakipeleka shuleni maana muda wa kula anakua hayupo nyumbani anakua yupo shuleni", alisema Mhe. Mwema.
Matarajio na dhamira ya wajumbe wa kikao hicho ni kuhakikisha mwaka huu wa fedha ni kuona kata zote zikifanya vizuri katika utekelezaji wa mkataba huo kwa kuhakikisha watoto wote wanapata angalau mlo mmoja wakiwa shuleni lengo ni kuboresha afya ya wanafunzi na kuongeza usikivu wa wanafunzi hao wawapo darasani.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa