Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Ndg. Mufandii Msaghaa, ametoa rai kwa wafanyakazi Wilayani Kiteto kufanya kazi kwa kujituma na kutenda haki.
Rai hiyo imetolewa kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo kiwilaya yamefanyika Aprili 30,2025 katika ukumbi wa Chama cha Walimu wilayani hapa.
Aidha Ndg. Msaghaa amewasihi pia wafanyakazi hao kua na tabia njema, wasikivu na wavumilivu katika utendaji wao wa kazi na haswa pale wanapotoa huduma kwa wananchi. “Wananchi wanatukimbilia kwa mambo mengi, tunapoonesha tabia mbaya tunaharibu sifa ya ofisi zetu”, ameongeza kiongozi huyo.
Mbali na hayo Katibu Tawala huyo alisisitiza upendo na ushirikiano baina ya mtumishi na mtumishi, idara na idara na hata taasisi kwa taasisi kwani ushirikiano unasaidia kutenda kazi kwa haraka na kusukuma gurudumu la maendeleo ya taifa.
Hotuba ya kiongozi huyo ilimalizikia kwa kuhamasisha kulinda amani haswa katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kutoa wito kwa wafanyakazi kushirikia katika uchaguzi na kuchagua viongozi bora.
Maadhimisho hayo ambayo yalianza kwa maandamano ya amani, yalihitimishwa kwa kugawa vyeti kwa wafanyakazi hodari kutoka kwenye taasisi mbalimbali wilayani hapa. Kauli Mbiu katika maadhimisho ya mwaka huu ni "Uchaguzi Mkuu 2025, Utuletee Viongozi Wanaojali Haki na Maslahi ya Wafanyakazi, Sote Tushiriki".
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa