Mkurugenzi wa miradi wa TEA Ndg. Waziri Rajab Salum akimkabidhi Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto nyaraka zinazohusu ujenzi kama ishara ya makabidhiano ya nyumba za walimu zilizojengwa na kampuni ya Watumishi Housing (WHC) kwa ufadhili wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).
Maafisa kutoka TEA na WHC, Wataalamu kutoka Halmshauri ,uongozi wa shule ya sekondari Lesoit pamoja na uongozi wa kijiji cha Lesoit wakikagua nyumba za walimu kabla ya makabidhiano
Nyumba za walimu ( 6 kwa 1) zilizojengwa na Watumishi Housing Company kwa ufadhili wa Mamlaka ya elimu Tanzania( TEA) katika muonekano wake wa mbele.
Nyumba za walimu ( 6 kwa 1) zilizojengwa na Watumishi Housing Company(WHC) kwa ufadhili wa Mamlaka ya elimu Tanzania( TEA) katika muonekano wake wa nyuma.
Mkurugenzi wa Miradi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Ndg. Waziri Rajab Salum akisaini nyaraka wakati wa makabidhiano ya nyumba za walimu katika shule ya sekondari Lesoit.
Mhandishi wa kampuni ya Watumishi Housing ( WHC) Mhandisi L.J Mwandobo akisaini nyaraka wakati wa makabidhiano ya nyumba za walimu.
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya wilaya ya Kiteto Ndg. Tamim Kambona akisaini nyaraka wakati wa makabidhiano ya nyumba za walimu
Kaimu Mhandisi wa ujenzi ( W) Mhandisi Chogo Magera akisaini nyaraka katika makabidhiano hayo
...............HABARI KAMILI..................
Mamlaka ya elimu Tanzania (TEA) wamekabidhi jengo lenye nyumba 6 kwa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto.Makabidhiano hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki katika shule ya msingi Lesoit ambapo ndipo zilipojengwa nyumba hizo.
Nyumba hizo ambazo zimejengwa na ‘Watumishi Housing Company’(WHC) zimekabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto mahususi kwa ajili ya kuishi walimu wa shule ya sekondari Lesoit.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo Mkurugenzi wa miradi wa TEA ndugu Waziri Rajab Salum ameipongeza ‘Watumishi Housing Company’ kwa kazi nzuri waliyoifanya, sambamba na kuwapa muda wa mwezi mmoja kurekebisha mapungufu madogo madogo ambayo yameonekana wakati wa kukagua nyumba hizo.
Aidha ndugu Waziri ametoa maelekezo kwa mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Lesoit Mwalimu Peter Nada kuhakikisha kwamba walimu wanahamia na kuishi katika nyumba hizo mapema iwezekanavyo. Akisisitiza kuhusu nyumba hizo kuanza kutumika ndugu Waziri anasema “kimsingi nyumba ziko vizuri na ziko tayari kwa ajili ya kuwasaidia walimu wetu wanaokaa mbali waweze kukaa karibu na wanafunzi wao .Marekebisho ambayo tumekubaliana kwamba WHC watayafanya,naamini watayafanya, na watayakamilisha ndani ya mwezi mmoja, wakati marekebisho hayo yakiwa yanendelea,walimu waingie waendelee kuishi katika nyumba hizi.”.
Kwa upande wake Mhandisi wa WHC ndugu L.J. Mwandobo amezishukuru mamlaka zote ambazo wameshirikiana wakati wote wa utekelezaji hadi kukamilika kwa mradi huo.Vilevile amewashukuru walimu na serikali ya kijiji kwa ushirikiano waliouonyesha wakati wote.Mhandisi Mwandobo amesema kwamba mara nyingi kazi za ujenzi huwa zinaambatana na wizi wa vifaa ,hususani kusipookuwa na serikali ya kijiji makini katika kulinda mali ambazo ni za serikali ,vitu vingi huwa vinapotea,hali inayosababisha serikali isifikie malengo katika miradi husika,lakini kwa Lesoiti hali imekuwa tofauti,kwani hakukuwa na upotevu wa kifaa chochote cha ujenzi.
Kuhusu mapungufu yaliyoonekana wakati wa kukagua nyumba hizo kabla ya makabidhiano, mhandisi Mwandobo amesema ,” Ninaamini kwamba sisi ‘Watumishi housing’ pamoja na mamlaka ya elimu(TEA) tutaweza kuweka utaratibu,kuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda kama ambayo tulivyokuwa tunatarajia”.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto ndugu Tamim Kambona amewashukuru TEA kwa ujenzi wa nyumba hizo, ndugu Tamim amesema “ Kwanza niwashukuru sana TEA, kwa ufadhili huu waliotufanyia, Kwa kweli wametukomboa ,tulikuwa na nyumba moja tu ya mwalimu, hapa Lesoit, sasa tutakuwa na nyumba saba za walimu,kwa hiyo changamoto ya uhaba wa nyumba za walimu kwa kiasi kikubwa imepungua.Kwa hiyo ningeomba na maeneo mengine pia watusaidie, kama tulivyoona kwenye yale mabweni na madarasa kwamba yanahitaji ukarabati mkubwa”.
Kadhalika kaimu mhandisi wa ujenzi wilaya ya Kiteto Mhandisi Chogo Magera amepongeza kazi iliyofanyika . Sambamba na pongezi hizo Mhandisi Magera ametoa rai kwa TEA kwamba wakati mwingine watakapokuwa na miradi katika wilaya ya Kiteto watumie wahandisi wa Halmashauri kwani wana uwezo wa kufanya kazi nzuri na kwa gharama nafuu.
Katika hatua nyingine mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Lesoiti ndugu Wilson Ranjili, amewashukuru TEA pamoja na ‘Watumishi Housing Company’ kwa kazi kubwa waliyoifanya kuwajengea nyumba nzuri sana. Na kwamba anaamini kwamba itakuwa ni chachu ya kuinua kiwango cha taaluma katika shule hiyo,kwani walimu wataishi katika mazingira mazuri , karibu na shule, hivyo ari ya ufundishaji itaongezeka.
Kabla ya makabidhiano hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto alitembelea maeneo mbalimbali ya shule ya Lesoit , maeneo hayo ni mabweni ( bweni moja la wasichana na bweni moja la wavulana, madarasa na maabara ya somo la kemia na baiolojia), ambapo katika mabweni hayo amejionea hali ya uchakavu wa dari na sakafu za mabweni hayo , ndipo akatoa maelekezo kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo kuitisha kikao cha bodi ya shule, kutathmini gharama inayotakiwa kutumika , ili ukarabati wa kuweka gipsam na sakafu katika mabweni hayo uanze mara moja.
.........MWISHO.............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa