Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, CPA Hawa Abdul Hassan ameipongeza timu ya wakusanya mapato ya Halmashauri kwa kazi kubwa na kujituma kwao, hatua iliyofanikisha ukusanyaji wa mapato kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 kwa kiwango cha asilimia 127.
Akizungumza katika kikao maalum cha mapato kilichofanyika wilayani Kiteto Septemba 23, 2025, CPA. Hawa alisema ufanisi huo umeifanya Halmashauri ya Kiteto kushika nafasi ya kwanza kwa ukusanyaji mapato katika Mkoa wa Manyara. Alisema mafanikio hayo yanatokana na mshikamano, uadilifu na bidii ya timu ya ukusanyaji mapato.
“Leo tumekutana kwa lengo la kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya. Nawapongeza sana kwa kujituma. Mafanikio haya ni ushahidi kuwa tukizingatia maadili ya kazi, tukiwa waaminifu na kushirikiana, tunaweza kufanikisha kila jambo,” alisema CPA Hawa.
Katika kikao hicho, watu nane waliotambuliwa kama.wakusanyaji bora wa mapato kwa mwaka 2024/2025, walikabidhiwa vyeti vya pongezi pamoja na zawadi ya fedha taslimu ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wao katika kuongeza mapato ya Halmashauri. Vilevile wakusanya mapato wengine wote walipatiwa vyeti vya pongezi kwa kazi nzuri waliyoifanya ya ukusanyaji wa mapato.
Hata hivyo, watendaji hao waliwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wakati wa utekelezaji wa kazi. CPA. Hawa aliahidi kuwa ofisi yake itazifanyia kazi changamoto hizo, akibainisha kuwa nyingine zinaweza kutatuliwa haraka na nyingine zinahitaji mipango ya muda mrefu.
“Nawaomba muwe wavumilivu, kwa sababu si kila tatizo linaweza kutatuliwa kwa haraka,” alisisitiza CPA. Hawa.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wakusanya mapato kuwa waadilifu na waaminifu, akisisitiza kuwa uaminifu wao ndio msingi wa mafanikio endelevu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mapato Wilaya ya Kiteto,Ndg. Prisca Mjema aliwasihi watendaji hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuepuka makosa yanayoweza kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa