Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akihutubia wananchi kwa niaba ya mgeni rasmi(Makamu wa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ) katika uzinduzi wa jukwaa la wanawake .
Wanawake wakiandamana kutoka katika ofisi ya Mkuu wa wilaya kuelekea uwanjani( chini ya mti) kwa ajili ya uzinduzi wa jukwaa la wanawake wilaya ya Kiteto.
Mwakilishi wa mgeni rasmi katika uzinduzi wa jukwaa la wanawake wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akikagua bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na vikundi vya wanawake wajasiliamali.
Diwani wa viti maalumu Kibaya Mhe. Zamzam Msabi akisoma risala ya wanajikwaa kwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa jukwaa la wanawake wilaya ya kiteto uliofanyika katika mji mdogo wa Kibaya.Aliyesimama upande wake wa kulia ni diwani wa viti maalum Loorela Mhe. Esta Lemahati.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi katika uzinduzi wa jukwaa la wanawake (Makamu wa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan). baada ya kukabidhiwa zawadi maalumu kwa ajili ya mgeni rasmi.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akizawadiwa na wanajukwaa katika uzinduzi wa jukwaa uliofanyika katika mji mdogo wa Kibaya .
......... HABARI KAMILI............
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa jukwaa la wanawake wilaya ya Kiteto ambaye amemuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan, mkuu wa wilaya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa amesema kwamba wakati umefika sasa jamii ibadili tabia na kutathmini mchango wa wanawake katika kuleta maendeleo katika familia na taifa kwa ujumla.Mhe Magessa ameyasema hayo wakati wa uzinduzi huo ambao umefanyika katika mji mdogo wa Kibaya mapema wiki hii.
Akizungumza wakati wa hotuba yake Mhe. Magessa amesema kwamba, kwa muda mrefu mwanamke amekuwa akionekana kama chombo cha kuzalisha mali,mtu asiye na sauti mbele ya mwanaume,na mlezi wa watoto. Lakini mwanawake ana mchango mkubwa sana katika kuleta maendeleo ya familia na taifa, malezi ya watoto na familia ,uzalishaji mali na kuinua pato la familia na taifa. Na kwa kuzingatia hilo,wanawake na wasichana wanastahili kupata elimu kama wavulana au wanaume wanavyopata elimu, na kupata ajira kama wavulan wanaume wanavyopata ajira, na wana haki ya kupata mgawanyo wa mali kama wanaume .Pia Mhe Magessa amaesema kwamba wanawake wanastahili kushiriki katika maamuzi.Akisisitiza kuhusu hilo Mhe ,Magessa amesema ‘‘ Pamoja na imani zetu za dini, mila na desturi zetu, wanawake washiriki katika maamuzi”.
Kadhalika Mhe. Magessa amezungumzia suala la malezi ya watoto ,ambapo amesema kwamba malezi ya watoto ni jukumu la wazazi wote wawili( baba na mama). Hivyo ni vema wazazi wote wawili kuwa karibu na watoto ili kufahamu matatizo yao na kuwafundisha maadili mema. Sambamba na hayo, amelitaka jukwaa la wanawake kuhakikisha kwamba linashirikiana na wanaume ili kutokomeza tatizo la mimba za utotoni, tatizo ambalo linakwamisha maendeleo ya watoto wa kike.
Katika risala yao kwa mgeni rasmi, wanajukwaa hao wametaja mambo makubwa matatu ya kuzingatia ili kupata maendeleo,Mambo hayo ni; kila mtu kuwa na maono ya kufika mbali katika maendeleo yake kuanzia katika ngazi ya familia, Kuthubutu na kuwa na ujasiri wa kujaribu jambo analoliamini kwamba litamtoa kutoka mahali alipo na kwenda katika hatua nyingine ya maendeleo na kuwa na moyo wa kujituma katika kutafuta maendeleo, ikiwa ni pamoja na kujiunga katika vikundi mbalimbali vya wajasiriamali.
Aidha wamesema kwamba uzinduzi wa jukwaa hilo utachangia kuwepo kwa fursa za ajira kwa wanawake na vijana.Uzinduzi huo unaenda sambamba na kauli mbiu isemayo ‘kuelekea uchumi wa viwanda , tuimarishe usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi’.Kauli mbiu ambayo inasisitiza juu ya umuhimu wa kutowabagua wanawake na kuwawezesha kushiriki katika shughuli mabalimbali za kiuchumi ili kujiletea maendeleo.
Uzinduzi wa jukwaa hilo ulianza kwa maandamano ambayo yalianzia katika ofisi ya mkuu wa wilaya(Bomani) na kuishia uwanjani (maarufu kama chini ya mti).Jukwaa la wanawake wilayani Kiteto lilianzishwa mwezi Mei 2017 na mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Tumaini Magessa,lengo likiwa ni kuwakutanisha wanawake pamoja ili waweze kujadili fursa,changamoto na kushiriki kikamilifu katika biashara na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa