Ufaulu wa mitihani ya Kidato cha Nne katika Halmshauri ya Wilaya ya Kiteto umeongeza na kufika 90.6% kutoka 90%.
Hayo yameelezwa February 16, 2024 na Mkuu wa Idara ya Sekondari, Ndugu Ally Kichuri katika Kikao Kazi cha Tathmini ya Matokeo ya Mitihani kilichofanyika katika Ukumbi wa Maktaba wilayani hapo.
Kikao hicho pia kiliambatana na Hafla ya utoaji wa Vyeti vya Pongezi kwa shule zilizofanya vizuri pamoja na kwa walimu waliofaulisha vizuri masomo yao katika matokeo ya mitihani hiyo iliyofanyika Novemba 2023.
Mgeni Rasmi katika Hafla hiyo alikua ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Mh Abdala Bundala ambaye aliongozana na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii WIlayani hapo, Mh. Kassim Msonde.
Mh. Bundala, aliwapongeza watendaji wote katika sekta ya elimu kwa kuongeza ufaulu huo. Pia Mh. Bundala alitoa rai kua waliofanya vizuri wapongezwe na waliofanya vibaya pia waambiwe ukweli.
Mbali na hilo Mh. Bundala alisema kwamba, sekta ya elimu ni eneo ambalo linashika nafasi kubwa kwenye kuitangaza Halmashauri ambapo inaweza kuitangaza vizuri ama vibaya kutokana na matokeo ya mitihani ya Taifa.
“Hata tufanye vizuri kwenye mapato kama kwenye elimu hatufanyi vizuri tutaonekana wa hovyo”, aliongeza Mh. Bundala.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, CPA. Hawa Abdul Hassan, aliwapongeza watendaji hao katika sekta ya elimu kwa kuongeza ufaulu na kusema kwenye matokeo ya mitihani ongezeko la 0.6% ni kubwa na anathamini jitihada zao ambazo zimepelekea ongezeko hilo la ufaulu.
Mbali na hayo Mkurugenzi aliwasihi watendaji hao kuendelea kupanga mikakati mizuri ya kuendelea kuongeza zaidi ufaulu katika shule zao.
“Mikakati iwe mizuri yenye tija na yenye kutekelezeka. Msiishie kupanga tu, bali na kutekeleza hiyo mikakati” aliongeza CPA. Hawa Abdul Hassan.
Vyeti vya pongezi vilivyotelewa kwenye hafla hiyo ilikua ni pamoja na pongezi za kufuta daraja sifuri ambapo vyeti hivyo vimetolewa kwa shule mbili ambazo ni Magungu na Engusero ilhali shule ya Orkine Partimbo na Magungu zilipokea vyeti vya pongezi kwa kuongeza Ufaulu kwa Miaka Mitatu Mfululizo. Shule ya sekondari Bwakalo ilipata cheti cha pongezi kwa kuongeza ufaulu kwa mika mitatu mfululizo kwa upande wa mitihani ya kidato cha pili.
Aidha Kiteto na Engusero zilipokea vyeti vya kuwapongeza kwa kuendelea kufanya vizuri katika kidato cha sita ambapo zimeendelea kufaulisha kwa 100%.Vilevile Kiteto ilipata tena cheti cha pongezi kwa kufaulisha 51% ya wanafunzi daraja la I-III.
Kikao hicho cha Tathmini kilihudhuriwa na Wakuu wa shule za sekondari wote, walimu wa taaluma kutoka katika shule hizo, Maafisa Elimu Kata; wataalamu wa Idara ya Elimu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi, wataalamu kutoka Ofisi ya Mdhibiti Ubora na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Kiteto.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa