Vituo vya Rasilimali kwa Walimu au kwa jina maarufu Vituo vya kujiendeleza walimu (Teachers' Resources Center - TRC) ni chachu muhimu ya kuinua kiwango cha elimu nchini Tanzania. Kupitia vituo hivi, walimu hupata nafasi ya kujiendeleza kielimu, kujifunza mbinu mpya za ufundishaji na kushirikishana uzoefu.
Pia, TRCs ni maeneo ambayo hutumika kufanya mikutano ya kitaaluma ambapo walimu hukaa pamoja kujadili changamoto zinazojitokeza kwenye ufundishaji na ujifunzaji na kutafuta mbinu bora za kuzitatua kupitia MEWAKA (Mpango Endelevu wa Mafunzo ya Walimu Kazini).
Wilayani Kiteto, tayari kuna TRC mbili zinazofanya kazi katika maeneo ya Shule ya Msingi Engusero na Kaloleni ambapo katika kituo cha Kaloleni kuna walimu 27 wanaojiendeleza kielimu katika ngazi ya Diploma na Shahada ya Kwanza kupitia elimu ya masafa ( Open Distance Learning).
Hivi karibu, halmashauri imeanza ujenzi wa vituo vingine viwili katika kata ya Songambele na kata Lengatei. Hatua hii ni kielelezo cha dhamira ya serikali na wadau wa elimu kuhakikisha walimu wanakuwa na mazingira rafiki ya kujengeana uwezo na kuboresha mbinu za ufundishaji.
Agosti 16, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, CPA. Hawa Abdul Hassan, alitembelea mradi ya ujenzi wa TRC katika eneo la Shule ya Msingi Orkine iliyopo katika kata ya Songambele ili kujionea hatua zilizofikiwa. Mradi huu una thamani ya shilingi milioni 50 kutoka Serikali Kuu.
Ziara yake ililenga kufuatilia maendeleo ya ujenzi na kuhakikisha kuwa kituo hicho kinakamilika kwa wakati ili kiweze kuanza kutoa huduma zinazotarajiwa.
Kwa uwepo wa TRC hizi, walimu Wilayani Kiteto watakuwa na jukwaa la pamoja la kujadili changamoto, kubadilishana uzoefu na kupata fursa ya mafunzo endelevu ya kitaaluma. Hii itasaidia kuinua ubora wa ufundishaji na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Mikakati iliyopo ni kuhakikisha kila Taarafa inakua na angalau kituo kimoja. Hakika, ujenzi wa TRCs katika wilaya ya Kiteto ni hatua muhimu ya kuwekeza katika walimu ambao ndiyo msingi wa mafanikio ya elimu na mustakabali wa taifa.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa