Katika mwendelezo wa maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yanayoendelea kufanyika kwenye viwanja vya Themi Njiro, agosti 6,2025 tukio la paredi ya mifugo limefanyika kwa shamrashamra kubwa likihusisha mifugo mbalimbali kutoka wilaya na taasisi mbalimbali za Kanda ya Kaskazini.
Mgeni Rasmi katika tukio hilo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, ambaye ametumia jukwaa hilo kutoa wito mahsusi kwa wafugaji kushiriki kikamilifu katika zoezi la utambuzi wa mifugo linaloendelea kitaifa.
Mhe. Mwema amesema kwamba zoezi hilo linahusisha uwekaji wa hereni za kielektroniki kwa wanyama kama ng’ombe, mbuzi na kondoo huku lengo likiwa ni kuongeza thamani ya ngozi ili iweze kumudu soko la kimataifa kwani kwa kutumia uwekaji alama ule wa awali umekua ukishusha thamani ya ngozi kwenye soko la kimataifa.
Mbali na hilo, zoezi hili linalenga kurahisisha ufuatiliaji wa afya ya mifugo, kuimarisha usalama dhidi ya wizi na upotevu, na kuwezesha biashara ya mifugo ndani na nje ya Tanzania kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta ya mifugo moja ya mikakati ni ni hili zoezi ambalo linalenga kuhakikisha kuwa mifugo inatambuliwa rasmi na inalindwa dhidi ya magonjwa hatari.
Aidha, Mgeni Rasmi huyo amewahimiza wafugaji kushiriki kikamilifu katika zoezi la chanjo kwa mifugo yao ili kuhakikisha afya bora na tija katika uzalishaji.
“Natoa wito kwa wafugaji kushiriki kikamilifu kwenye zoezi hili. Ushiriki wenu sio tu unalinda afya ya mifugo bali unachangia usalama wa chakula, uchumi wa kaya na maendeleo ya taifa kwa ujumla,” ameongeza Mhe. Mwema.
Kwa upande wa Wilaya ya Kiteto, zoezi la utambuzi wa mifugo limeanza rasmi tarehe 5 Agosti 2025 katika Tarafa ya Kibaya. Zoezi hilo limeanza kwa mafunzo kwa maafisa mifugo kutoka kata zote za tarafa hiyo, ambao baadaye watakwenda kutekeleza shughuli hiyo katika maeneo yao ya kazi.
Paredi ya mifugo imeendelea kuwa kivutio kikubwa katika maonesho ya mwaka huu, ikionesha si tu uzalishaji bora wa mifugo bali pia jitihada za serikali na wadau katika kuboresha sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Mifugo iliyoshiri katika paredi hiyo ni wanyama wa maziwa, wanyama kwaajili ya nyama, wanyama kazi(punda na farasi) pamoja na wanyama walinzi(mbwa).
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa