Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti akijibu kero mbalimbali zilizowasilishwa na wakazi wa kata ya Engusero katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Engusero wilayani Kiteto.
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akifafanua jambo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Engusero.
Diwani wa kata ya Engusero Mhe. Solomoni Mbulunyuku akifafanua jambo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Engusero.
Waheshimiwa madiwani ,wakuu wa taasisi mbalimbali za serikali , kamati ya ulinzi na usalama ,kamati ya siasa pamoja na wakuu wa idara na vitengo wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Engusero wilayani Kiteto.
Wakazi wa kata ya Engusero wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Engusero wilayani Kiteto .
Wakazi wa kata ya Engusero wakiwasilisha kero zao kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Engusero wilayani Kiteto.
...... HABARI KAMILI.......
Viongozi wa Ngazi za Chini Simamieni Utekelezaji wa Maagizo - RC Mnyeti
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mheshimiwa Alexander Mnyeti amewataka viongozi wote walio chini yake kusimamia utekelezaji wa maagizo yote anayoyatoa na yanayotolewa na viongozi wengine wa juu wa serikali.Mheshimiwa Mnyeti ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Engusero wilayani Kiteto.
Akizungumza katika mkutano huo Mhe. Mnyeti amesema kwamba Kiongozi anapotoa maagizo ni vema viongozi walio chini yake wakayasimamia na kuyatekeleza ili kuondoa malalamiko ya wananchi.Akisisitiza kuhusu utekelezaji wa maagizo Mhe. Mnyeti anasema ‘‘ Yale ambayo tutakubaliana katika mkutano huu nitayafuatilia kuhakikisha kwamba yanazingatiwa na kufanyiwa kazi kwa wakati ili wananchi wasiendelee kupata shida. Inawezekana kabisa kwamba viongozi walishakuja hapa na kutoa maagizo,lakini utekelezaji wa maagizo hayo haukuzingatiwa na viongozi wa ngazi za chini. Mimi leo niko hapa maelekezo nitakayoyatoa hapa, naamini viongozi wote mlio chini yangu mtayazingatia na kuyasimamia kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapungukiwa kero walizonazo”.
Vilevile Mhe. Mnyeti amesema kwamba viongozi wanatakiwa kushughulikia kero za wananchi na kuzipatia majibu katika muda sahihi ili wananchi wasiendelee kuelemewa na kero . Akisisitiza kuhusu viongozi hao kushughulikia shida za wananchi ,Mhe. Mnyeti anasema ‘‘Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametuelekeza viongozi wote wa ngazi za chini tuhakikishe tunashughulika,tunahangaika na shida za watu’’ .
Katika hatua nyingine Mhe. Mnyeti amewahakikishia wananchi hao kuwa maagizo yote aliyoyatoa katika mkutano huo yatasimamiwa na yatatekelezwa.Akisisitiza kuhusu hilo Mhe. Mnyeti anasema ‘‘ Mimi niwatoe wasiwasi wananchi , na niwahakikishie kwamba Awamu hii viongozi wote lazima wafanye kazi zao.Na kila mtu lazima ahakikishe amekaa kwenye mstari wa kazi yake.Akishindwa kutimiza wajibu wake, ni bora akapumzika ,akatafutwa mtu mwingine ambaye anaweza akafanya kazi kwa ajili ya watu’’.Mhe. Mnyeti pia amesema kwamba wananchi ndio waajiri wa viongozi, na ndio waliowaweka madarakani hivyo wana wajibu na wanapaswa kusema kile ambacho wanadhani viongozi wao wanaweza wakakifanya.Na viongozi wasiofanya yale wananchi wanayoyataka, hao sio viongozi wanaofaa . Aidha Mhe. Mnyeti amesema kwamba yeye kwa niaba ya Mhe. Rais atahakikisha anafuatilia shida za wananchi na zinatafutiwa majibu katika muda muafaka.
Katika mkutano huo kero zilizojitokeza ni kutotekelezwa kwa baadhi ya ahadi za viongozi wanaofika katika kata hiyo, mwananchi kulalamika shamba lake kugeuzwa njia ya n’gombe (Palio), wafugaji kulishia mifugo katika mashamba ya wakulima na mkulima kupigwa na kuporwa pesa zake na vijana wa kifugaji na baadae kufunguliwa mashtaka. Ambapo Mheshimiwa Mnyeti ameahidi kuzipatia ufumbuzi kero hizo ndani ya muda mfupi, na ametoa maelekezo kwa viongozi wa chini kuhusu namna ya kutatua kero hizo.
......... MWISHO.........
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa