Septemba 16, 2025, Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto ilifanya semina elekezi kwa watumishi wa ajira mpya wa wilayani hapa, yenye lengo la kuwajengea uelewa kuhusu wajibu wao, maadili ya kazi na namna bora ya kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya taifa na jamii kwa ujumla.
Katika semina hiyo, mada mbalimbali ziliwasilishwa kutoka taasisi na idara tofauti za serikali. Afisa kutoka Idara ya Uhamiaji Konstebo Anthony Mapunda aliwapatia elimu ya namna ya kuwatambua wasio raia wa Tanzania na kuwatahadharisha kutokutoa barua za utambulisho kwa watu wasiowajua kwa lengo la kuzuia udanganyifu na upatikanaji holela wa hati za kusafiria.
Aidha, Afisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bi. Mwanaisha Juma alitoa somo kuhusu madhara ya rushwa, ambapo watumishi hao walipewa onyo dhidi ya kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu.
Vilevile, Afisa kutoka Shirika la Hifadhi ya Jamii (PSSSF) Ndugu. Harrison Werema aliwasilisha elimu kuhusu mafao mbalimbali ambayo wanachama wake hunufaika nayo, ikiwemo mafao ya uzeeni, matibabu, pamoja na mafao mengine ya kijamii.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Rasilimali Watu wa Halmashauri, Ndg. Rose Massay aliwafundisha watumishi hao kuhusu stahiki zao kisheria pamoja na wajibu wao wa kila siku katika utumishi wa umma.
Mbali na elimu hizo, mada kuhusu maadili ya utumishi wa umma pia ilitolewa, ambapo watumishi wapya walihimizwa kuzingatia maadili na kuishi kama kioo cha jamii hata wanapokuwa nje ya maeneo ya kazi. Vilevile watumishi hao wapya walipewa elimu juu ya matumizi ya mfumo wa utendaji kazi (PEPMIS).
Akifungua rasmi semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Remidius Mwema, aliwasihi watumishi hao kuwa mfano wa kuigwa kwa wananchi na kuhakikisha wanastawi na kustahimili mazingira yoyote waliyopangiwa kwa uadilifu na moyo wa kujitolea.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto CPA. Hawa Abdul Hassan, alifunga semina hiyo kwa kuwataka watumishi hao wapya kutumia mafunzo waliyoyapata kama dira ya kazi.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa