Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto CPA. Hawa Abdul Hassan, wakati akihitimisha mafunzo elekezi ya Watumishi wa Ajira mpya yaliyofanyika Septemba 16,2025.
Akizungumza na waajiriwa wapya CPA. Hawa amewataka waajiriwa hao kuwa makini na mahusiano yao binafsi ili kuepuka kuathirika na maambukizi ya UKIMWI, amesisitiza kuwa ugonjwa huo bado ni tishio kubwa katika jamii.

“Naomba nitumie fursa hii kuwakumbusha kulinda afya na kuhakikisha mnapima afya zenu kabla ya kuanzisha mahusiano mapya kwani UKIMWI bado upo na ni vigumu kumtambua muathirika kwa macho”,alisisitiza CPA.Hawa
Aidha, CPA.Hawa aliwaonya kutokukimbilia mikopo kutoka taasisi zisizo rasmi maarufu kama vibanda umiza, kwani mikopo hiyo huwa na riba kubwa inayoweza kuathiri utendaji wao kazini na kudhoofisha ustawi wa kifamilia.
Hata hivyo, CPA. Hawa aliwasisitiza watumishi hao kuwa na nidhamu ya matumizi ya pesa na kuepuka mikopo isiyo na lazma na pale inapobidi kukopa waende kukopa kwenye taasisi rasmi za kifedha ambako masharti yapo wazi.
Mbali na hilo, CPA. Hawa aliwasihi kujiandaa mapema kwa maisha ya baada ya kustaafu kwa kuwekeza katika mifuko mbalimbali ya uwekezaji. Vilevile, aliwahimiza waepuke ulevi, walinde mienendo yao na waendelee kushikilia maadili kazini na nje ya kazi.

Pia aliwashauri waajiriwa hao wapya kutoridhika na viwango vya elimu walivyonavyo bali kuhakikisha wanajiendeleza kimasomo na kitaaluma ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia ya sasa.
Awali, CPA. Hawa aliwakaribisha rasmi waajiriwa hao na kuwataka kutimiza wajibu wao kwa uadilifu, huku akiwahakikishia kuwa mwaajiri hatasita kuwapatia haki zao kwa mujibu wa sheria na taratibu za ajira.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa