Afisa Mwandikishaji Jimbo la Kiteto, CPA. Hawa Abdul Hassan, amewaasa Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata kufanya kazi kwa ueledi na uaminifu.
Rai hiyo imetolewa Septemba 18, 2024 katika Ufunguzi wa Mafunzo ya Maafisa Waandikishaji Wasaidizi Ngazi ya Kata Kuhusu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo maafisa hao kwenye ujazaji wa fomu mbalimbali ambazo zitatumika kwenye zoezi la uboreshaji wa Daftari pamoja na kujengewa uwezo wa utumiaji wa mifumo na vifaa vya uandikishaji.
"Naamini mtafanya kazi kwa ueledi, bidii na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hili na kuweza kufikia malengo", amesisitiza Afisa Mwandikishaji huyo.
Aidha amesema kwamba kila mmoja wa Maafisa hao anawajibika kutunza vifaa watakavyo tumia kwani vimenunuliwa kwa gharama kubwa na vitahitajika kufanya kazi katika majimbo mengine.
Kabla ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Maafisa hao Waandikishaji Wasaidizi Ngazi ya Kata, waliapa kiapo cha Uaminifu na Kutunza Siri katika zoezi hilo. Kiapo hicho kimetolewa mbele ya Hakimu wa Wilaya Mhe. Mossy Soro Sasi.
Mara baada ya kupewa mafunzo hayo ya siku mbili, Maafisa hao wanatarajiwa kuendesha mafunzo kama hayo kwa Waandishi Wasaadizi na Waendesha Mashine za BVR.
Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Jimbo la Kiteto linatarajiwa kuanza Septemba 25 hadi Oktoba 1, 2024.
"Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura, ni Msingi wa Uchaguzi Bora".
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa