Wachimbaji wa machimbo ya madini ya dhahabu katika machimbo ya Ilndorokon yaliyopo kata ya Njoro wameomba kuchimbiwa kisima ili kuwawezesha kupata maji kwa bei nafuu.
Akiongea Mei 6, 2024 mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mh. Remidius Mwema, mmoja wa wachimbaji hao Ndg Thomas Masuke alisema kwamba dhahabu inahitaji maji mengi na kwa sasa wachimbaji hao wanaingia gharama kubwa kwani wananunua lita 20 za maji kwa gharama ya TZS 1,500.
Kutokana na kero hiyo Masuke aliomba wachimbiwe kisima katika eneo hilo ili waweze kupata maji kwa gharama nafuu.
Mbali na kero ya maji wachimbaji hao pia walilalamika kuhusu ubovu wa barabara inayoelekea eneo hilo la uchimbaji na hivyo kumuomba Mh. Mkuu wa Wilaya kuwasaidia pia kwenye eneo la barabara.
Aidha Mchimbaji Gullam Tambwe aliomba wachimbaji waruhusiwe kutumia vifaa vya kisasa “compressor” katika uchimbaji wa dhahabu katika machimbo hayo ili kuongeza tija tofauti na sasa ambapo wanalazimika kutumia vifaa duni.
“Mimi nimeleta compressor kutoka Dar es Salaam kwaajili ya uchimbaji ila baada ya kufika hapa imezuiwa tunaambiwa hatutakiwi kutumia hiyo mashine ila hatujui sababu. Ombi langu tunaomba turuhusiwe kutumia kompresa” aliongeza Gullam.
Mbali na hayo wachimbaji hao waliomba pia huduma za afya katika eneo hilo.
Kuhusiana na changamoto ambazo zinahusisha wachimbaji na muwekezaji wa eneo hilo, Mh. Mwema ameahidi kuitisha kikao kati yake na muwekezaji halisi wa eneno hilo na sio muwakilishi wake pamoja na wawakilishi wachache wa wachimbaji hao ili wakae pamoja na kutatua changamoto hizo.
“Najua nae angekuwepo hapa huenda ana yake kuhusu wachimbaji. Lazma kuwepo mazingira ambayo yatalinda haki za pande zote mbili yaani mwenye leseni ya uchimbaji na wachimbaji” ameongeza Mh. Mwema.
Kuhusiana na changamoto ya maji, Mh. Mwema amesema hiyo ni fursa kwa mtanzania yoyote ambaye anaweza kuchimba kisima katika eneo hilo anaweza fanya hivyo.
“Changamoto zenu nimezisikia nyingine siwezi kuzipatia ufumbuzi hapa, ninazichukua nikaongee na timu yangu nitarudi tena kwa mrejesho” aliongeza Mh. Mwema.
Machimbo ya Ilndorokon yalianza rasmi April 15,2024 na mpaka sasa eneo hilo lina watu wapatao 320.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa