Timu ya wataalamu kutoka Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Mei 22,2024 imetembelea Wilaya ya Kiteto na kufanya kikao kujadili changamoto zilizojitokeza katika uuzaji wa zao la mbaazi kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani katika msimu uliopita.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mh. Remidius Mwema, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto CPA. Hawa Abdul Hassan, wajumbe wa Kamati ya Fedha, wataalamu wa kilimo kutoka ofisi ya Mkoa na kutoka Wilayani Kiteto, pamoja na maafisa ushirika wa Wilayani hapo.
Katika kikao hicho, wadau hao walijadili changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika uuzaji wa zao la mbaazi katika msimu ulipita na kujadili njia za kutatua changamoto hizo ili kuziepuka katika msimu huu.
Kati ya changamoto zilizojitokeza katika msimu uliopita ni pamoja na upungufu wa maghala ya kutosha katika vyama vya msingi vya mazao na masoko yenye kukidhi vigezo vya kuhifadhia mazao, uelewa mdogo wa wakulima kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani na uwepo wa walanguzi/madalali ambao walikua wananunua mbaazi moja kwa moja kutoka kwa wakulima.
Aidha changamoto nyingine ni kutokuwepo na mageti ya kutosha kwenye mipaka ya wilaya ya Kiteto ili kuzuia utoroshwaji wa mbaazi kutoka nje ya wilaya na pia baadhi ya vyama vya msingi kutokua tayari kuingia kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani.
Katika kutatua changamoto ya utayari wa vyama vya msingi, wajumbe walikubaliana maafisa ushirika wakae na vyama vya msingi wajue kuhusu utayari wao kuingia kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani na pale itakapoonekana hawapo tayari, ijulikane nani atafanya kazi kwa niaba yao.
Aidha wajumbe wamekubaliana kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu mfumo huo kwani katika msimu uliopita zoezi lilianza mwishoni wa msimu na hivyo hakukua na muda wa kutosha wa kutoa elimu hiyo kwa wakulima.
Vilevile imejadiliwa kuwekwa mageti ya kutosha haswa maeneo ambayo yanapakana na wilaya nyingine ili kudhibiti utoroshwaji wa mbaazi.
Kuhusu changamoto ya maghala, Bi Sura Ngatuni, Meneja wa Mipango na Uhamasishaji WRRB, amesema kwamba WRRB itatuma wataalamu kukagua maghala ya watu binafsi ili kubaini kama yanakidhi vigezo ili yaweze kuongezwa kwaajili ya kurahisha ukusanyaji wa mbaazi.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa