Wafugaji wa mbwa wilayani Kiteto wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kuwaleta mbwa na paka wao ili kupata chanjo dhidi ya kichaa cha mbwa katika maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani ambayo Kitaifa yanayotarajiwa kufanyika wilayani Kiteto Septemba 26-29, 2025.
Daktari wa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Dkt. Lunonu Sigalla amesema maandalizi ya maadhimisho hayo yanaendelea vizuri, na Kiteto inatarajiwa kupokea wataalamu wa mifugo zaidi ya 100 kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Afya, Shirika la Kilimo na chakula (FAO) na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA). Pia watakuwepo wataalumu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Halmashauri na Mikoa mbalimbali pamoja na wadau kutoka sekta binafsi kwaajili ya maadhimisho hayo.
“Kwa siku tatu, kila asubuhi timu zetu za wataalamu zitatawanyika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hii kutoa huduma za chanjo na elimu. Hii ni nafasi muhimu kwa wafugaji wote kuhakikisha mbwa na paka wao wanapata chanjo na huduma nyingine zitakazotolewa bila gharama yoyote”, amesema Dkt. Sigalla.
Mbali na chanjo, huduma nyingine zitakazotolewa bure ni pamoja na kuhasi mbwa na paka dume na kutoa kizazi kwa mbwa na paka jike. Aidha, kutatolewa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuhusu utaratibu wa chanjo za kichaa cha mbwa, namna ya kujikinga na maambukizi ya kichaa cha mbwa na hatua za haraka za kuchukua iwapo mtu atang’atwa na mbwa.
Dkt. Sigalla ameongeza kuwa chanjo ni kinga madhubuti na nafuu zaidi ikilinganishwa na gharama kubwa za matibabu ya binadamu anaposhambuliwa na mbwa mwenye kichaa.
“Kiteto kuwa wenyeji wa maadhimisho haya Kitaifa ni fursa ya kipekee sana, hivyo tunatoa wito kwa wafugaji wote wajitokeze na kuwaleta mbwa pamoja na paka wao katika maeneo yatakayotangazwa. Hii ni nafasi ya kulinda wanyama na familia zetu dhidi ya madhara makubwa ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa”, amesisitiza Dkt. Sigalla.
Maadhimisho haya yanatarajiwa kuwa fursa ya pekee kwa jamii ya Kiteto sio tu kupata huduma hizo bure bali pia kuongeza uelewa juu ya afya ya wanyama ili kujenga jamii salama.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa