Zaidi ya wagonjwa 400 waliogundulika kua na ugonjwa wa trakoma/vikope wamepatiwa matibabu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto katika mpango maalumu ya kutokomeza ugonjwa huo wilayani hapo.
Hayo yamebainishwa na Mtaalamu wa Macho wilayani hapo, Ndg. Enock Thomas Awary Mei 29, 2024 katika Zahanati ya Dongo iliyopo wilayani hapo wakati wa matibabu ya ugonjwa huo katika kata ya Dongo.
Mtaalamu Awary amesema wagonjwa hao ni kati ya wagonjwa 1768 waliokisiwa ambao mpango huu ulidhamiria kuwapatia matibabu katika utekelezaji wa mradi huu ambao ulianza mwishoni mwa mwaka 2022 na unatarajiwa kuisha Desemba 2024.
Aidha, ilibainishwa kwamba mpango huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Halmashauri ya Wilaya Kiteto pamoja na shirika la kimataifa liitwalo Helen Keller ambapo shirika hilo linagharamia matibabu hayo bure kwa wagonjwa ikiwemo pamoja na kuwachukua nyumbani kwa ajili ya matibabu na usafiri wa kurudi nyumbani mara baada ya matibabu. Aidha shirika hilo linagharamia mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii wanaohusika na zoezi la awali la kubaini waathirika wa vikope. Mafunzo hayo yanahusisha elimu juu ya ugonjwa huo kwa jamii na elimu ya uchunguzi wa awali kwa wanakaya.
Akitoa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa huu, Mtaalumu huyo amesema kwamba Trakoma au ugonjwa wa vikope ni aina ya ugonjwa wa macho unaosababishwa na vimelea aina ya bakteria unaoenezwa na inzi wadogo kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Mtaalamu huyo ameongeza kwamba, mtu aliyepata maambuzi ya ugonjwa huo, kope zake moja au zaidi ya moja hujikunjia kwa ndani na hugusa katika kioo cha mbele cha jicho. Hali hii humfanya mgonjwa wa vikope kusikia maumivu ya jicho na kufanya ahisi kama jicho limejaa mchanga.
Mtaalamu Awary ameeleza kwamba ugonjwa huo hauna dawa bali hutibiwa kupitia usawazishaji wa kope ambao katika wilaya hiyo hufanywa katika zahanati zilizopo kwenye kata kwa ratiba maalumu.
“Kama leo tupo hapa katika Zanahati ya Dongo kuendesha zoezi la usawazishaji wa kope baada ya kuwabaini wagonjwa. Usawazishaji huu tunaufanya kwa kuchana kidogo katika kifuniko cha jicho na kisha kushona kwa nyuzi. Matokeo ya usawazishaji wa vikope ni kwamba kope zikiota zitakuwa zinasimama kwenda juu na kurudia katika hali ya kawaida hivyo kutogusa tena kioo cha mbele cha jicho”, amesema Mtaalamu huyo.
Sababu za ugonjwa wa Trakoma/vikope ni kutofanya usafi wa uso, kutofanya usafi wa mazingira na kutumia kipande cha nguo kimoja kufuta macho ya mzazi na mtoto. Aidha imeelezwa kwamba jamii ya wafugaji ipo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa wa trakoma.
Mtaalamu Awary pia ameeleza kwamba ugonjwa huu wa vikope usipotibiwa haraka unaweza kusababisha upofu kwani kope zikiendelea kugusa kwenye kioo cha mbele cha jicho kwa muda mrefu, husababisha kovu katika kioo cha jicho.
Elimu ndogo kwa jamii juu ya ugonjwa na matibabu ya usawazishi wa kope haswa kwa jamii ya ufugaji ni moja ya changamoto katika utekelezaji wa mradi huu kwani wapo baadhi ya wagonjwa ambao hawapo tayari kufanyiwa usawazishaji wa kope.
Aidha mtaalamu huyo ameongeza kwamba kuhamahama kwa makazi pia kunakwamisha matibabu kwani timu ya wataalamu wanapoenda kwenye nyumba ya mgonjwa kwaajili ya kumchukua kwenda kwenye matibabu wanakuta mgonjwa alishahama makazi na wanashindwa kupata taarifa mahali alipohamia mgonjwa.
Nae Ndg. Allen Lemilia, Afisa Mradi kutoka Helen Keller, ameshukuru kwa ushirikiano kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara pamoja na na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kiteto kwa kuwapa nafasi timu ya madaktari kuweza kufika vijijini na kutoa matibabu kwa wagonjwa wa vikope.
"Pia niombe jamii ya watu wa Kiteto waendelee kujitokeza pale wanaposikia taarifa za kambi za matibabu zinazoendelea hapa wilayani na wapuuze baadhi ya watu wanaowaogopesha kwamba ukitibiwa macho yanaharibika kwani usawazishaji wa vikope hutumia vifaa bora na salama kwa jicho", ameongeza Ndg. Lemilia.
Tafiti za awali zimeonesha kuwa kuna wagonjwa wanaohitaji huduma za usawazishaji wa vikope ili wasipate upofu wa kudumu takribani 2,441 katika mkoa wa Manyara huku Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto ikiongoza kwa kuwa na wagonjwa 1,768.
Mpango huu wa matibabu ya vikope unaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt..Samia Suluhu Hassan za kuthamini afya za wananchi na kusogeza huduma za afya karibu.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa