Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akizungumza na wakazi wa kata za Kibaya, Kaloleni na Bwagamoyo ,katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji mdogo wa Kibaya mwishoni mwa wiki.
Diwani wa kata ya Kibaya Mhe. Kasim Msonde akifungua mkutano .
Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto akizungumza katika mkutano huo.
Wakuu wa idara mbalimbali za halmashauri ya wilaya ya Kiteto wakipunga mkono kama ishara ya kuwasalimia wananchi katika mkutano huo.
Afisa Ardhi (W) ya Kiteto Ndg. Damas Gulisha akitoa maelekezo kuhusiana na taratibu zinazotakiwa kufuatwa ili mwananchi aweze kumiliki ardhi.
Mkuu wa Kituo kituo kikuu cha polisi Kibaya Patric Kimaro akitoa ufafanuzi kuhusiana na kero iliyowasilishwa na mmoja wa wakazi wa kibaya waliohudhuria mkutano huo.
Wananchi wakiwa wamekusanyika katika mkutano huo kumsikiliza Mkuu wao wa wilaya.
Wananchi wakiwasilisha kero zao wakati wa mkutano huo.
.....HABARI KAMILI......
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mheshimiwa Tumaini Magesa amewataka wakazi wa Kiteto kutojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa sheria kwani kwa kufanya hivyo serikali itawachukulia hatua kali.Mhe. Magesa ametoa angalizo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji mdogo wa Kibaya, wilayani Kiteto mwishoni mwa wiki.
Akizungumza wakati akihutubia mkutano huo Mhe. Magessa amesema kwamba Kuna ujangili unaendeshwa Kibaya, ambapo watu wanakwenda maeneo ya Makame ,wanawinda digidigi ,wanawaleta Kibaya wanatumika kama kitoweo, na watu wengine wameonekana wakiuza mishikaki ambayo inasadikika kwamba ni ya digidigi. Mhe Magessa amewaonya watu wanaojihusisha na uuzaji wa nyama ya digidigi ,ikiwemo mishikaki , kwamba waache mara moja tabia hiyo,kwani serikali itaendesha operesheni maalumu kwa ajili ya kukabiliana na vitendo hivyo vya ujangili. Akisisitiza kuhusu angalizo hilo Mhe Magessa amesema “kazi inaanza leo,ukikamatwa utaingia kwenye mikono ya sheria kwa sababu unafanya ujangili.Ninajua kabisa kwamba kuna watu siku nyingi hawaendi kwenye mabucha ,wanakula nyama pori ambazo zinawindwa kinyume cha sheria, tutawakamata, na tutawapelekeka kwenye vyombo vya sheria, watashughulikiwa ipasavyo”.
Sambamba na suala la ujangili Mhe. Magessa ameonya kuhusu uchimbaji madini usiofuata sheria. Hapa Mhe. Magessa anasema “Kuna ndugu zetu hapa hapa Kibaya, wamekuwa wakiondoka wanatafuta madini kila mahali, kwa hiyo kila mahali sasa, watu wanavizia wanalipua baruti wanatafuta madini.Hili nalo liwe na utaratibu, ziko leseni kama unataka kuchimba madini,ambazo unatakiwa uwe nazo ili uweze kufanya hizo shughuli za uchimbaji madini.Sio kila mahali watu wanapiga baruti tu .Kuna watu wanabaruti humu,na kazi yake ni hiyo,wanakwenda wakilipua katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kutafuta madini , na wanapopiga baruti wanyama waliopo katika maeneo hayo wanakimbia. Sasa hili tuelezane tu kama wananchi, tusije tukaingia katika mtego ambao mtu unavuja sheria ya nchi,na baadae ukikamatwa inaonekana kama unaonewa’’.
Kadhalika Mhe .Magessa amezungumzia suala la elimu ambapo amesema kwamba kila mzazi ama mlezi mwenye mtoto ambaye amefikia umri wa kwenda shule ,kuhakikisha kwamba mtoto huyo anaandikishwa kwa ajili ya kuanza shule, na kwamba ni lazima kufanya hivyo, na mzazi au mlezi ambaye hatampeleka mtoto wake shule atakamatwa na kushtakiwa kwa kutompekeka mtoto shule. Mhe Magessa amewasisitiza wakazi wa Kiteto kulipa kipaumbele suala la elimu kwa ajili ya manufaa ya baadae ya watoto wao, wao wenyewe wazazi, jamii na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Magessa pia amezungumzia suala la chaneli za televisheni ambazo zilikuwa zikionekana katika visimbuzi vya DSTV, ZUKU na AZAM ambazo kwa sasa hazionekani katika visimbuzi hivyo.Mhe. Magessa ametoa ufafanuzi kuhusiana na suala hilo ambapo amesema kwamba urushaji wa chaneli za televisheni unafanyika kulingana na leseni ambazo kampuni zinazohusika na urushaji wa chaneli za televisheni kwa mfumo wa kidigitali zinakuwa zimepewa na tume ya mawasiliano. Na kwamba ziko leseni za kurusha chanel bure, na zipo leseni za kurusha chaneli kwa kulipia tu. Hata hivyo kampuni hizo zimekuwa zikirusha kwa kulipia ,chaneli hizo ambazo kwa mujibu wa sheria za tume ya mawasiliano zinatakiwa zirushwe bila kulipia, kwamba kisimbuzi kinapokuwa hakijalipiwa,au muda uliolipiwa umeisha, chaneli zinazotakiwa kuonyeshwa bure, zimekuwa hazionekani.
Mhe. Magessa ameendelea kusema kwamba tume ya mawasiliano ilikuwa na kesi ambayo ilikuwa imefunguliwa baina yake na wamiliki wa kampuni hizo ambazo zimekuwa zikikiuka utaratibu kwa kuonyesha chaneli za bure kwa kulipia, na baada ya kesi hiyo kumalizika,wakatakiwa kunyang’anywa leseni zao,na ili wasinyanganywe leseni hizo,wakaamua kuziondoa chaneli zote za bure. Mhe. Magessa amesema kwamba ni vema wananchi wakafahamu kwamba chaneli hizo hazitarudi hadi kampuni hizo zitakapokuwa na leseni zinazowaruhusu kuonyesha chaneli za bure.
Aidha Mhe Magessa pia ametoa ushauri kwa wakazi wa Kiteto ambao wana visimbuzi hivyo ambavyo chaneli za bure hazionekani , kwamba waendelee kuvitumia kwa sababu vina maudhui ambayo wanayapenda, lakini pia wafanye utaratibu wa kupata visimbuzi vya Star Times, TING, Digtec na Continental ili waweze kuona chaneli za bure ambazo ndizo zinazoonyesha mambo mengi yenye maudhui ya ndani ya nchi, hususani habari, matukio na kazi mbalimbali zinazofanywa na serikali yao.
Katika hatua nyingine Mhe. Magessa amezungumzia suala la migogoro ya ardhi ambapo amesema kwamba kumekuwa na mlundikano wa migogoro ya ardhi, migogoro hiyo imetokana na migongano katika umiliki wa ardhi. Mhe Magessa amesema kwamba utaratibu wa namna gani mtua anatakiwa kupata ardhi ameusema zaidi ya mara moja,lakini inaonekana bado watu hawajaelewa ndio sababu migogoro inaendelea.Hapa akamtaka afisa ardhi wa wilaya ya Kiteto ndugu Damas Gulisha kuwaeleza wananchi taratibu ambazo zinatakiwa kufuatwa iki kuweza kupata umiliki wa ardhi,ambapo ndugu Gulisha ametoa maelezo ya kina kuhusiana na taratibu hizo.
Ili kuhakikisha kwamba migogoro yote ya ardhi wilayani inafika idara ya ardhi, Mhe. Magessa amewaagiza wenyeviti wa vijiji wote kuorodhesha watu wenye matatizo ya ardhi wote na kuyapeleke idara ya ardhi,ambapo wataalamu wa ardhi watafika kila mahali panaposemwa pana mgogoro ili kutatua migogoro hiyo.
Mhe. Magessa amesema kwamba migogoro mingi imekuwa haipatiwi ufumbuzi kutokana na kwamba watu wamekuwa wanakwenda mahali ambako sio sahihi.Kwamba iko idara ya ardhi ambayo ina wataalamu wa kutosha kushughulika na masuala ya ardhi,kama mtu ana mgogoro wowote unaohusu ardhi, majibu yote atayapata idara ya ardhi.Na kama atakuwa hajaridhika afike ofisini kwake au ofisini kwa DAS ili migogoro hiyo iweze kutatuliwa na hatimaye wilaya iweze kuwa na amani na utulivu.Mhe. Magessa pia amesema kwamba ziko fomu ambazo wenyeviti wa vijiji/mitaa wanatakiwa wawe nazo, zinaitwa sema usikike,kwamba kama mtu ameshindwa kueleza maelezo yake kwa mkuu wa wilaya, anataka kuyaeleza kwa waziri, atajaza hiyo fomu, itatumwa kwenda kwa waziri,waziri akishaisoma atamjibu.Na kwamba wakifanya hivyo migogoro itakuwa inakwisha kwa usalama,badala ya vile ambavyo imekuwa ikiisha kwa magomvi.
Mhe. Magessa amefanya mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Kibaya,mkutano huo umehusisha kata tatu ambazo ni Kibaya,Kaloleni na Bwagamoyo.Mkutano huo ni wa kawaida, ambao lengo lake ni Mkuu wa wilaya kutoa maelekezo ya serikali, kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.
.......MWISHO.......
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa