WAKULIMA WA MBAAZI WILAYANI KITETO WAPATA KICHEKO
Wakulima wa zao la mbaazi wilayani Kiteto wamefurahishwa na mfumo mpya wa uuzaji wa zao hilo kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani baada ya zao hilo kununuliwa kwa bei ya shillingi 2261 kwa kilo moja kupitia mnada wa kwanza.
Katika mnada huo ambao umeendeshwa Septemba 5,2023 na Chama Kikuu cha Ushirika Arusha (ACU) katika kata ya Matui, jumla ya tani 250 za mbaazi zimenunuliwa. Jumla ya makampuni sita yalijitokeza kuomba kununua mbaazi hizo hata hivyo kampuni ya SM Holding LTD ndio iliyoshinda katika mnada huo.
Mmoja ya wakulima ambao walipeleka mbaazi ghalani kwaajili ya kuuzwa kwa mnada, Bwana Mohamedi Said Kidevu aliishukuru serikali kwa kuleta mfumo huo maana hauna usumbufu na pia wameuza kwa bei nzuri ambayo hata wangeamua kusafirisha zao hilo wakauzie Dar es Salaam wasingeweza kuuza kwa bei hiyo.
Akiongea katika mnada huo, Meneja wa ACU Bwana Innocent Kisole alitoa rai kwa wakulima wote kujiunga katika vyama vya msingi.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kiteto SSI Mbaraka Alhaj Batenga ambaye ndiye aliyekua mgeni rasmi katika mnada huo alisema kwamba serikali haiwezi kuweka pesa kwenye mfuko wa kila mwananchi ila badala yake serikali inachokifanya ni kuweka mazingira mazuri ya watu kuinuka kiuchumi.
“Katika mazao changamoto ilikua ni kukosa soko ila Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuja na mfumo huu kilimo sasa kimekuja kumkomboa mwananchi. Kila mtu asimame kwenye nafasi yake vizuri” aliongeza Mh Batenga.
Pia Mh Batenga alitoa onyo dhidi ya watu ambao watajaribu kuchezea ushirika na ameagiza kwamba mbaazi zote zinazolimwa Kiteto ziuzwe kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kiteto Mh. Abdala Bundala alisema kwamba mfumo wa stakabadhi ghalani umekuja mkombozi wa wakulima na pia umekuja kama mkombozi kwa Halmashauri kwa kukusanya mapato pasipo kukimbizana.
Katika mnada huo Kampuni ya SEDACO iliomba kununua kwa bei ya shilingi 2105 kwa kilo, HS LTD iliomba kununua kwa bei ya shilingi 1900 kwa kilo na Kampuni ya YURI iliomba kununua kwa bei ya shilingi 2050. Kampuni ya Export Trading iliomba kununua kwa bei ya shilingi 2168 na kampuni ya Afrishan iliomba kununua kwa shilingi 2250.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa