Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Uchumi , Diwani Mussa Braiton, ametoa rai kwa watumishi wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kuwajulisha wananchi kuhusu uwepo wa huduma ya upimaji wa afya ya udongo.
Hayo ameyasema katika Kikao Cha Robo ya Pili cha Kamati ya Huduma za Uchumi kilichofanyika Februari 16, 2024 katika Ukumbi wa Halmashauri.
Diwani Braiton amesema kwamba serikali imeleta kifaa cha kupimia afya ya udongo na pia imewawezesha Maafisa Ugani pikipiki ili kurahisha zoezi hilo, hivyo wananchi wanapaswa wajue upatikanaji wa huduma hiyo.
“Wananchi wajulishwe na wapewe elimu kuhusu upimaji wa afya ya udongo” aliongeza Diwani Braiton.
Nae Mwenyekiti wa Halmashauri, Mh. Abdala Bundala, amesisitiza kwamba jambo la kupima afya ya udongo lichukuliwe kwa umuhimu mkubwa ili kuweza kuongeza uzalishaji haswa katika kipindi hiki ambacho uzalishaji unashuka.
Huduma ya upimaji wa afya ya udongo hutolewa bure na ili mwananchi aweze kupimiwa afya ya udongo katika shamba lake, anapaswa kupeleka ombi lake kwa Afisa Ugani kisha Afisa huyo ataenda kwenye shamba la mkulima na kuchukua sampuli ya udongo na kwenda kuipima katika maabara iliyopo katika Ofisi za Idara ya Kilimo Kiteto.
Baada ya majibu ya afya ya udongo kutoka, mkulima anashauriwa aina sahihi ya mbolea ya kutumia ili kurutubisha ardhi ya shamba lake.
Toka Halmashauri ipokee kifaa cha kupimia udongo Agosti 2023, jumla ya sampuli 312 za udongo kutoka katika vijiji 15 vilivyopo katika kata za Bwawani, Matui, Chapakazi, Ndirigishi, Olboroti, Njoro na Partimbo zimepimwa afya yake na ushauri stahiki wa matumizi ya ardhi hizo umetolewa kulingana na majibu ya afya ya udongo katika vijiji husika.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa