Mwezeshaji wa mafunzo ya awali ya mipango na bajeti ya masuala ya lishe ngazi ya halmashauri bibi Stella Sasita akielekeza kuhusiana na mambo ya msingi ya kusisitiza wakati wa uandaaji wa bajeti katika mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa hospitali ya wilaya ya Kiteto mwishoni mwa wiki.
Mwezeshaji wa mafunzo Ndg. William Mambo akielekeza kuhusana na mfumo wa Plan Rep na mabadiliko yaliyofanyika.
Afisa lishe ( W) ya Kiteto Bibi Beatrice Rutanjuka akiwasilisha taarifa yake ya shughuli za lishe kabla ya kuanza kwa mafunzo.
Washiriki wa mafunzo wakiwa katika picha ya pamoja,mara baada ya kumaliza mafunzo.
.......HABARI KAMILI .......
Wakuu wa idara zinazohusika na masuala ya lishe katika Halmashauri ya wilaya ya Kiteto wametakiwa kushirikiana katika uandaaji wa bajeti ya shughuli za lishe.Kauli hiyo imetolewa na muwezeshaji wa mafunzo ya awali ya mipango ya bajeti ya masuala ya lishe ngazi ya halmashauri bibi Stella Sasita wakati wa kikao kazi cha mafunzo hayo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hospitali ya wilaya mwishoni mwa wiki.
Akisisitiza kuhusu umuhimu wa ushirikiano katika uandaaji wa bajeti na mipango kazi ya shughuli za lishe Sasita amesema “ Mipango iwe ya ushirikiwaji.Wakuu wa idara mshirikiane, ushirikishwaji unaondoa kujirudia rudia kwa shughuli katika mipango kazi. Kwamba kama mwenzako amepanga kutekeleza shughuli fulani,kwa sababu amekushirikisha, wewe hutaiweka tena kwenye mpango wako,utaweka shughuli nyingine’’.
Sasita pia amefundisha kuhusu mambo muhimu yanayotakiwa kutiliwa mkazo wakati wa uandaaji wa bajeti na mipango ya shughuli za lishe, Sasita amesema kwamba ili kupanga ni lazima kuwa na takwimu.Takwimu ni muhimu sana . Kuwa na malengo ambayo ni ‘SMART’ kwa maana kwamba malengo yanatakiwa kuwa maalum,yanayopimika,yanayotekelezeka,yawe na uhalisia na muda maalumu wa utekelezaji.
Aidha Sasita ameelekeza kwamba shughuli zote zinazohusiana na masuala ya lishe zinatakiwa zilenge kwenye lengo J. Si hivyo tu, bali shughuli zote za masuala ya lishe ambazo zitapangwa , ni lazima pia zilenge kusaidia utekelezaji wa mkataba uliosainiwa na Katibu Tawala wa Mkoa. Sasita amesema kwamba mambo ya kufanya ni mengi sana ,na kwamba kikao hicho ni cha utekelezaji,kinahitaji matokeo hivyo wakuu hao wa idara waongeze bidii zaidi ili kuweza kupata matokeo chanya katika utekelezaji wa shughuli za lishe.
Naye mwezeshaji William Mambo ameeleza kuhusu mabadiliko yaliyofanywa katika mfumo wa Plan Rep ambapo amesema kwamba mwaka wa fedha uliopita shughuli nyingi za lishe zilikuwa katika lengo C, lakini baada ya mabadiliko shughuli hizo kwa sasa zipo katika lengo J. Na kwamba afisa mipango ana jukumu la kuhakikisha kwamba taarifa zote zinaingia kwenye mfumo.Amesisitiza kuwa ni lazima wakuu wa idara pamoja na maafisa bajeti wote kujua kwamba shughuli zao zinatekelezwa kwenye nini. Mambo pia amekazia kuhusu suala la ushirikano,ambapo amesema kwamba wakuu wa idara na maafisa bajeti washirikiane wakati wa kuandaa bajeti, ili kuwa na uhakika kwamba shughuli walizokusudia kuzitekeleza zimeingizwa kwenye mfumo.
Katika hatua nyingine Afisa lishe wa wilaya ya Kiteto bibi Beatrice Rutanjuka amesisitiza kuhusu mabadiliko katika ufuatiliaji wa bajeti,ambapo amewataka wakuu wa idara kuhakikisha kwamba hawaishii tu kwenye kupanga bajeti ya shughuli za lishe katika idara zao, bali pia wawe wafuatiliaji kuhakikisha kwamba fedha zilizotengwa zinapatikana, na utekelezaji wa shughuli unafanyika kama inavyoonekana katika mipango yao.
Vilevile Rutanjuka amezungumzia kuhusu suala la kujituma ,amesema kwamba ni muhimu sana kila mmoja kujituma ili mambo yaweze kwenda,kwani bila ya kuwa na moyo wa kujituma hakuna jambo lolote litakalofanikiwa .
Mafunzo hayo ya siku moja yamelenga katika kuzijengea uwezo kamati za lishe , kupanga na kusimamia masuala ya lishe ngazi ya wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania Bara.
.........MWISHO..........
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa