Walezi na wamiliki wa vituo vya kulea watoto wadogo mchana (Daycare Centres) wilayani Kiteto wamehimizwa kua mstari wa mbele katika kupambana na ukatili wa kijinsia wilayani hapo.
Rai hiyo imetolewa Agosti 30, 2023 na Mgeni Rasmi , Dr. Vicent Gyunda alipokua akifunga mafunzo ya siku kumi kwa walezi na wamiliki wa vituo hivyo wilayani hapo.
Dr. Gyunda ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Wilaya, alisema kwamba katika mafunzo hayo washiriki walifundishwa namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia na jinsi ya kuwatambua waathirika wa matukio hayo, hivyo baada ya mafunzo hayo Halmashauri inaamini sasa inaenda kujenga jamii nzuri maana wahitimu hao wanaenda kua mabalozi katika kutoa elimu na kupambana na ukatili.
Mbali na hayo Dr Gyunda alisema kwamba baada ya mafunzo hayo wanategemea kuona malezi katika vituo vyao yanafuata misingi yote kama ambavyo wameelekezwa katika mafunzo hayo . Pia alisema kwamba anaamini kuwa wahitimu hao watakua mabalozi wa kuelimisha kuhusu umuhimu wa lishe shuleni.
“Tunaamini kwamba sasa mtahakikisha malezi kwenye vituo vyenu hayaingii doa ila pia tunategemea mtakua walinzi kwa kukemea pale ambapo mtaona mambo hayaendi sawa kwenye vituo ” aliongeza Dr. Gyunda.
Licha ya hayo, DR. Gyunda alisema kwamba wahitimu hao sasa wamebaki na kazi kubwa ya kusajiri vituo vyao kutokana na misingi na vigezo walivyofundishwa.
Katika risala ya wahitimu wa mafunzo hayo ambayo ilisomwa na Bw Enerick Mwambene, wahitimu hao waliushukuru uongozi wa Halmashauri kupitia Ustawi wa Jamii Wilaya kwa kua viungo muhimu katika kufanikisha mafunzo hayo.
Mbali na hilo wahitimu hao walieleza moja ya changamoto katika vituo vyao ni ukosefu wa miongozo ya kutumia katika vituo vya kulelea watoto wadogo mchana na hivyo kulazimika kutumia muongozo wa elimu ya awali. Katika kujibu hoja hiyo Mgeni rasmi alisema kwamba suala hilo wamelipokea na watalifanyia kazi.
Mafunzo hayo ambayo yameratibiwa na Ofisi ya ya Rais TAMISEMI pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wanawake na Makundi Maalumu; wilayani Kiteto yalihudhuliwa na washiriki 85 na yaliongozwa na Mkufunzi wa Kitaifa Bi Restituta Bujiku.
Nae Afisa Ustawi wa Wilaya Bi Jackline Barongo alisema kwamba lengo la mafunzo hayo ni kupunguza changamoto ya walezi wasio na sifa ya kulea na kufundisha watoto chini ya miaka mitano waliopo katika vituo vya kulea watoto wadogo mchana.
Nchini Tanzania, huduma ya vituo vya kulea watoto wadogo mchana inatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Watoto namba 21 ya mwaka 2009 ikiwa na lengo la kuwapatia watotot wadogo wenye umri chini ya miaka mitano malezi changamshi.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa