Afisa michezo wa mkoa wa Manyara ambaye pia ni mkufunzi wa mafunzo ya riadha kwa watoto 'Kids Athletics', Ndg. Charles Maguzu akizungumza wakati wa mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika uwanja Mkuu wa michezo Kibaya - Kiteto .
Walimu kutoka katika shuke mbalimbali wilayani Kiteto wakiwa tayari kuanza na mafunzo ya michezo ya riadha kwa watoto ' Kids Athletics'.
Walimu Rodgers Mvigilije wa shule ya sekondari Kiteto na Edna Tesha wa shule ya msingi Songambele wakitoa maoni yao kuhusiana na mafunzo waliyoyapata.
.......HABARI KAMILI.........
Walimu 91 wa shule za msingi na sekondari wilayani hapa wamepata mafunzo ya michezo mbalimbali .Mafunzo hayo ya siku 3 yamefanyika kwenye uwanja mkuu wa michezo katika mji mdogo wa Kibaya,wilayani Kiteto, ambapo yalifunguliwa rasmi siku ya Jumamosi 03/11/2018 na kufungwa jana Jumatatu 05/11/2018.
Akizungumza kuhusu mafunzo hayo,Afisa michezo wa mkoa wa Manyara ambaye pia ndiye mkufunzi wa mafunzo hayo, ndugu Charles Maguzu amesema “ Mafunzo haya niliyapata Dar es Salaam, chini ya Shirikisho la Michezo ya riadha la Dunia (IWF).Lengo la mafunzo haya ni kuwafundisha walimu michezo michezo ili waweze kwenda kufundisha michezo hiyo katika shule zao.Riadha ndio mchezo mama wa michezo yote,katika michezo yote ambayo tunacheza, watu lazima wakimbie,lazima waruke,lazima warushe.Ndani ya mchezo wa riadha matukio yote hayo yamo. Kwa hiyo tunawapa 'kids athletics program' ambazo zitatengeneza msingi wa kuwafanya waweze kufundisha michezo yote ,kwa ajili ya kukuza vipaji vya watoto”.
Aidha Maguzu ameeleza umuhimu wa michezo ambapo amesema kwamba michezo inaongeza nidhamu kwa wanafunzi mashuleni . Inawajenga kiafya. Inawajengea uwezo wa kujiamini na kuwa wadadisi wa mambo.Wanakuwa na uwezo wa kupambana katika mazingira yoyote yale.Michezo pia inajenga ushirikiano miongoni mwa wanafunzi wanapokuwa wanasoma. Na kwamba wanaposoma kwa ushirikiano,uelewa wao unakuwa mpana zaidi.Pia inajenga upendo kwa wanafunzi, kukutana pamoja na kucheza kunawafanya wajione kama ndugu.
Maguzu ameongeza kusema kwamba kila mwalimu aliyeshiriki katika mafunzo hayo, anatakiwa akafundishe wanafunzi wasiopungua 350,na kwa kufanya hivyo ,wanafunzi wengi katika wilaya ya Kiteto wataweza kupatiwa mafunzo hayo.anaamini kuwa walimu ambao wamepata mafunzo hayo wakiyapeleka kwa wanafunzi , kuanzia mwakani wilaya ya Kiteto itakuwa inatengeneza wanafunzi ambao wanavipaji na ujuzi wa kutosha kufanya vizuri katika UMITASHUMTA na UMISETA na kuiletea sifa wilaya yao.
Katika hatua nyingine Maguzu ametoa shukrani kwa Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi Mtendaji kwa kuhamashisha walimu kujitokeza kwa wingi kushiriki mafunzo hayo.Vilevile amewasifu walimu kwa kushiriki mafunzo vizuri, pamoja na kuonyesha nidhamu ya hali ya juu katika siku zote za mafunzo .
Sambamba na shukrani hizo amewaasa walimu kwamba baada ya kupata mafunzo hayo na kutunukiwa vyeti, wasiende kuvifungia kabatini na kutowafundisha watoto ,endapo watafanya hivyo ,watakuwa hawajayatendea haki mafunzo hayo, wala wanafunzi wao, na lengo la kushiriki mafunzo litakuwa halijatimia. Vilevile Maguzu ametoa wito kwa walimu waliohudhuria mafunzo hayo ambapo amesema kwamba wajipange wakati mwingine pia waweze kuhudhuria mafunzo.Na kwa kuwa wilaya ya Kiteto ni kubwa, hata kama wataamua kujipanga huko pembezoni mwa mji,atakuwa tayari kuja kuwafundisha, kwani lengo lake lengo ni kuwafikia walimu wengi , ili mafunzo hayo yawafikie watoto wengi zaidi.
Kwa upande wao walimu waliopata mafunzo hayo walikuwa na haya ya kusema;
Mwalimu Edna Tesha wa shule ya msingi Songambele amesema kwamba amefurahia sana mafunzo aliyoyapata ,kwani yamemsaidia kuimarisha afya yake, amejua uwezo wake katika michezo ,pia yamemsaidia kufahamu michezo mingi ambayo atakwenda kuwafundisha wanafunzi wake. Mwalimu Tesha anaamini kwamba michezo hiyo itawasaidia watoto kuwa imara, kuwa na akili ya kujifunza na kuelewa kwa haraka. Pia ameiomba Halmashauri chini ya Mkurugenzi ; mafunzo yatolewe mara kwa mara ili walimu wawe na ujuzi wa kutosha utakaowawezesha kuandaa kizazi chenye vipaji na ujuzi wa kucheza michezo mbalimbali.
Mwalimu Rogers Mvigilije wa shule ya sekondari Kiteto amesema kwamba mafunzo yalikuwa mazuri sana, wamejifunza vitu vingi , wamejifunza michezo mbalimbali, kila aina ya mchezo ambao watoto wanastahili kufundishwa wameugusa. Mwalimu Mvigilije pia amesema kwamba anaamini kuwa mafunzo waliyopata yataisaidia jamii. Vilevile ametoa rai kwamba mafunzo yawe endelevu, na kwamba Halmashauri iendeelee kuona ni kwa namna gani wakufunzi wa michezo wataendelea kuja Kiteto ili walimu waendeelee kupata ujuzi zaidi na zaidi kwa lengo la kuinua michezo wilayani.
..........MWISHO.........
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa